17 Mei 2024 - 13:02
Afisa Myahudi katika serikali ya Biden ajiuzulu kulalamikia mauaji ya kimbari ya Ghaza

Lily Greenberg Call, msaidizi maalumu wa mkuu wa wafanyakazi katika Idara ya Mambo ya Ndani ya serikali ya Marekani amekuwa mteuliwa wa kwanza wa kisiasa wa Kiyahudi kujiuzulu hadharani akipinga uungaji mkono wa Washington kwa mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika katika Ukanda wa Ghaza uliowekewa mzingiro.

Call amemshutumu Rais Joe Biden kwa kuwatumia Wayahudi kuhalalisha sera ya Marekani katika vita vya Israel.

Katika mahojiano na The Associated Press, afisa huyo wa Kiyahudi ameashiria matamshi kadhaa ya Biden, ikiwa ni pamoja na aliyotoa katika hafla ya White House Hanukkah ambapo alisema "kama isingwekuwapo Israel, kusingekuwa na Myahudi duniani ambaye angebaki salama".

Aidha, amegusia kauli ya rais huyo wa Marekani kwenye Kumbukumbu ya Holocaust iliyofanyika Washington wiki iliyopita ambapo alisema mashambulizi ya Oktoba 7 yaliyoongozwa na Hamas na 'kusababisha vita' yalichochewa na alichokiita "utashi wa tokea hapo kale wa kuwaangamiza Wayahudi."Lily Greenberg Call ameyakosoa matamshi hayo ya Rais wa Marekani akisema: "anawafanya Wayahudi sura ya mashine ya vita ya Marekani. Na hilo ni kosa kubwa sana," na akakumbusha kuwa mababu zake waliuliwa kutokana na "ghasia zilizofadhiliwa na serikali."

Katika barua yake ya kujiuzulu, afisa huyo maalumu wa Idara ya Mambo ya Ndani ya Marekani amesema: "siwezi tena kwa dhamiri njema kuendelea kuwakilisha utawala huu huku Rais Biden akiendelea kuunga mkono mauaji ya kimbari ya Israel...ni nini maana ya kuwa na nguvu za madaraka kama hutoyatumia kukomesha uhalifu dhidi ya binadamu?"

Kwa uchache, Call anakuwa ni afisa wa tano wa ngazi ya kati au ya juu wa Marekani kutangaza hadharani kujiuzulu kupinga uungaji mkono wa kijeshi na kidiplomasia wa utawala wa Biden kwa vita vya miezi saba vya mauaji ya kimbari vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ghaza, ambavyo hadi sasa vimepelekea kuuawa shahidi zaidi ya Wapalestina 35,000, wengi wao wakiwa watoto wachanga, watoto wadogo na wanawake - na kujeruhi zaidi ya 79,000. Wapalestina wengine 10,000 wanahofiwa kufukiwa chini ya vifusi vya majengo yaliyoripuliwa.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, licha ya kuendelea kukosolewa vikali hata ndani ya Marekani kwenyewe kwa kufadhili mauaji ya Wapalestina wa Ghaza, kwa mujibu wa duru mbili za Bunge, siku ya Jumanne utawala wa Biden ulianzisha hatua za awali za mchakato wa kufanikisha mpango mwingine mpya wa kuipatia Israel msaada wa silaha wenye thamani ya dola bilioni moja.../


342/