Osama Abdel Khalek balozi na mwakilishi wa kudumu wa Misri katika Umoja wa Mataifa alisema Jumanne ya jana tarehe 21 Mei kwamba, nchi yake inapinga vikali hujuma na uvamizi wa Israel dhidi ya mji wa Rafah na inasisitiza juu ya ulazima wa kusitishwa hujuma na mashambuliio hayo ya Israel. Abdel Khalek ameongeza kuwa, kuendelea hujuma na uvamizi dhidi ya Ukanda wa Gaza kutasababisha kusitishwa misaada ya kibinadamu na hatua za kibinadamu katika ukanda huo. Mwakilishi wa kudumu wa Misri katika Umoja wa Mataifa kadhalika amesema kuwa, kuna mambo yanayotokea huko Rafah ambayo ni jinai dhidi ya binadamu na kwamba, jamii ya kimataifa inabeba dhima na masuuliya ya hilo.
Vasily Nabenziya balozi na mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa, pia aligusia katika kikao hicho cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kifurishi cha dola bilioni 26 cha misaada ya Marekani kwa utawala wa Kizayuni na kubainisha kwamba, Tel Aviv inapokea makombora na mabomu mapya kwa ajili ya kuangamiza maisha ya Wapalestina. Katika radiamali yake kuhusiana na kuendelea jinai za utawala ghasibu wa Israel zinazofanywa huko Gaza kwa himaya na uungaji mkono wa madola Magharibi hususan Marekani, mwakilishi huyo wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa ametaka kuweko mashinikizo zaidi ya kimataifa dhidi ya Washington na Tel Aviv.Tangu kuanza mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza ambayo katika miezi ya hivi karibuni yamesababisha mauaji ya halaiki na kuharibiwa miundombinu ya kiuchumi na kiafya katika eneo hilo, nchi huru na zisizokubali kuburuzwa zimechukua hatua kubwa kukabiliana na Wazayuni katika uga wa kimataifa.
Mashtaka ya Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), yaliyopelekea kupendekezwa ombi la kutolewa hati ya kukamatwa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni na Waziri wa Vita wa utawala huo, ni matokeo ya hatua madhubuti zilizochukuliwa ambazo bila shaka ni mafanikio ya ushirikiano na uchukuaji wa hatua za pamoja za mataifa huru. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekasirishwa mno na hatua ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ya kutaka kutolewa hati ya kukamatwa kwake pamoja na viongozi wa Hamas kuhusu madai ya uhalifu wa kivita katika mzozo wa Gaza.
Kadhalika, kupitishwa kwa rasimu ya azimio la uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa ni miongoni mwa hatua zilizofikiwa na juhudi za nchi huru. Baada ya miaka mingi ya kuzuiwa na Marekani, hatimaye hivi karibuni Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipiga kura kuunga mkono rasimu ya azimio la uanachama kamili wa Palestina katika asasi hiyo.
Hotuba za wawakilishi wa Misri na Russia katika Umoja wa Mataifa, zilizowaunga mkono wananchi wa Palestina na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni, ni ishara ya kuundwa kambi mpya katika matukio ya kimataifa, ambapo Marekani na waungaji mkono wake wa nchi za Magharibi sio watoaji maamuzi wakuu katika hilo.Matukio ya Gaza baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa yamepelekea kuzidi kutengwa utawala wa Kizayuni na kuzingatiwa matakwa halali ya wananchi wa Palestina. Russia, China na Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zinazotilia maanani hali ya Palestina na watu wa Gaza katika siasa zao za nje na hazikubali propaganda za daima za nchi za Magharibi kuiunga mkono kikamilifu Tel Aviv. Utendaji wenye uratibu wa jamii ya kimataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni kwa namna fulani umekuwa ni natija ya sera madhubuti na athirifu za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuunga mkono haki halali za watu wa Palestina katika miaka ya hivi karibuni, ambayo imekuwa na nafasi nzuri katika kuifanya jamii ya kimataifa na nchi huru kuwa na uzingatiaji wa hali halisi ya mambo katika eneo.
342/