28 Mei 2024 - 16:54
Umoja wa Mataifa: Changamoto za ulimwengu zinaongezeka huku afya ikizorota

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, changamoto zinazoukabili ulimwengu hivi sasa zimekuwa zikiongezeka kila sikuu huku hali ya afya ikizorota.

Hayo yameelezwa na Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambapo ameliambia Baraza Kuu la 77 la Shirika Afya Duniani katika hotuba yake kwa njia ya video, kwamba dunia inakabiliwa na matatizo na kwamba afya ya ulimwengu inazorota kuanzia machafuko ya hali ya hewa hadi kuongezeka kwa umaskini na ukosefu wa usawa, na kuzidisha migogoro.

Baraza Kuu la 77 la Shirika Afya Duniani lilifungua kikao chake cha kila mwaka cha wiki nzima jana Jumatatu ambapo wajumbe wana jukumu la kuweka sera za afya kwa mwaka ujao huku kukiwa na changamoto kubwa kwa ustawi wa ulimwengu kutokana na migogoro mingi ambayo, katika baadhi ya maeneo inatishia pakubwa afya na maendeleo ya watu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, mamilioni ya watu nchini Sudan na Gaza wako katika hatari ya kufa, sio tu kutokana na risasi na mabomu, lakini kutokana na majeraha yasiyotibiwa na magonjwa.  Aidha ameeleza kuwa, mashambulizi yasiyo ya kawaida dhidi ya vituo vinavyotoa huduma za afya huenda kikawa ndio kitu kikubwa zaidi ambacho nimeshuhudia katika wakati wangu kama Katibu Mkuu”.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza juu ya udharura wa kuwekwa mipango madhubuti zaidi kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za afya zinazoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali duniani.

342/