20 Februari 2025 - 19:57
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu: Kupanua uhusiano na majirani ni sera ya uhakika ya Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: kupanua uhusiano na majirani ni sera ya uhakika ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, aliyasema hayo jana Jumatano katika mkutano na Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad bin Khalifa Al Thani na ujumbe aliofuatana nao na akabainisha kwamba: "moja ya sera zilizotangazwa za serikali ya Iran ni kupanua uhusiano na majirani zake, na kwa rehma za Mwenyezi Mungu zimefanyika kazi nzuri katika uga huu na mafanikio kadhaa yamepatikana."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, ana matumaini kuwa, makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa Iran na Qatar mjini Tehran yatazifaidisha nchi zote mbili na pande zote mbili zitaweza kutekeleza majukumu ya ujirani, zaidi ya ilivyokuwa hapo awali.

Katika mazungumzo hayo, Ayatullah Khamenei ameashiria pia matamshi ya Amir wa Qatar kuhusu masuala ya eneo na akaongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaitambua Qatar kuwa ni nchi rafiki na ndugu, ijapokuwa kungali kuna masuala yenye utata na ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi, kama vile kurejeshwa mali za Iran ambazo zilihamishwa kutoka Korea Kusini na kupelekwa Qatar; na kizuizi kikuu cha kutekelezwa makubaliano yaliyofikiwa juu ya suala hilo ni Marekani.

Kwa upande wake, Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad bin Khalifa Al Thani ameeleza furaha aliyonayo kwa kukutana na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu na akaipongeza misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya kuwaunga mkono wanaonyongeshwa duniani na wananchi wa Palestina.

Amir wa Qatar amemhutubu Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kumwambia: "kusimama kwako imara Muadhamu na bega kwa bega na wananchi wa Palestina hakutasahaulika katu".../

342/