20 Februari 2025 - 19:59
Wabunge EU: Ulaya haiwezi kuendelea kuitegemea Marekani

Wabunge wa Bunge la Ulaya wamesema bara hilo haliwezi kuendelea kuitegemea kikamilifu Marekani kwa ulinzi; na kutoa wito wa kuimarisha uwezo wa kiulinzi wa Ulaya sambamba na kuendelea kuiunga mkono Ukraine.

Katika taarifa ya pamoja siku ya Jumanne, mirengo mikuu ya Bunge la Ulaya—ikiwa ni pamoja na Chama cha Watu wa Ulaya, Wasoshalisti na Wademokrats, kundi la Renew Europe, na Greens—ilisisitiza kwamba Ulaya lazima ichukue jukumu kubwa zaidi kwa usalama wake na ulinzi wa mamlaka ya kujitawala Ukraine.

Taarifa hiyo inaashiria mabadiliko makubwa katika mtazamo wa kimkakati wa Ulaya, ikionyesha wasiwasi juu ya Marekani kutegemewa katika masuala ya usalama wa kimataifa na kuimarisha juhudi za kuimarisha uhuru wa Ulaya katika ulinzi na kuzuia mashambulizi dhidi yake.

Weledi wa mambo wanasema Umoja wa Ulaya unafuatilia kwa dhati kukomesha utegemezi wa ulinzi, wakati huu ambapo kunashuhudiwa mabadiliko ya vipaumbele vya sera za kigeni ya serikali mpya ya Marekani.

Hii ni katika hali ambayo, Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni alisema hivi karibuni kuwa, Umoja wa Ulaya haupaswi kuchukua msimamo ambao utakinzana na sera ya Marekani kuhusu Ukraine.

Viongozi wa nchi kadhaa za Ulaya walikutana Paris karibuni huku kukiwepo na wasiwasi uliochochewa na hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kuwasiliana na kuanzisha mazungumzo ya moja kwa moja na Russia na nia ya serikali yake ya kuitenga EU katika mazungumzo ya amani ya Ukraine.

342/