Taarifa iliyotolewa na ofisi hiyo imesema: "tumeona utawala ghasibu unavyoshadidisha uhalifu dhidi ya raia katika wiki za hivi karibuni, ukiwalenga makusudi watu wanaookota kuni au kukagua nyumba zao, na kusababisha vifo vyao kwa mashambulio ya jeshi la Israel".
Taarifa hiyo imetolewa baada ya shambulizi la anga la jeshi la utawala wa Kizayuni kulenga eneo la Beit Lahia kaskazini mwa Ghaza na kusababisha vifo vya Wapalestina tisa wakiwemo waandishi wa habari na wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu.
Ikilaani shambulio hilo ililolielezea kama "mauaji ya kutisha ya halaiki", Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Ghaza imeulaani utawala ghasibu wa Israel kwa kushadidisha uchokozi wake huku kukiwepo na ripoti kwamba kuna maagizo yanayotolewa mtawalia kutoka uongozi wa juu wa utawala huo wa Kizayuni ya kuchukuliwa hatua za kijeshi.
Ofisi hiyo imetupilia mbali madai ya jeshi la Kizayuni ya kuhalalisha mashambulio yake ikisema, watu waliolengwa, wote ni raia wanaofanya kazi katika eneo la utoaji hifadhi ya makazi, waliokuwa wakiandaa taarifa za taswira za vyombo vya habari kwa ajili ya shirika la utoaji sadaka.
Taarifa hiyo imeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) zichukue hatua za haraka dhidi ya uhalifu wa kivita wa Israel, ikiwa ni pamoja na ule uliofanywa na waziri mkuu wake Benjamin Netanyahu.
Tangu Oktoba 2023 hadi sasa, Wapalestina wasiopungua 48,500, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa shahidi kutokana na vita vya kinyama vya jeshi la utawala wa Kizayuni vilivyoligeuza magofu pia eneo la Ghaza.../
342/
Your Comment