16 Machi 2025 - 17:59
Source: Parstoday
Makundi ya Muqawama yalaani vikali jinai mpya za Marekani nchini Yemen

Harakati mbalimbali za Muqawama zimelaani vikali kwa kauli moja jinai zinazoendelea kufanywa na Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen, katika njama za Washington na London za kujaribu kuulinda utawala ghasibu wa Israel mbele ya operesheni za Sana’a zinazofanyika kama sehemu ya kuliunga mkono taifa madhlumu la Palestina.

Makundi hayo ya Muqawama yamelaani jinai hizo katika taarifa tofauti muda mfupi baada ya ndege za kivita za Marekani na Uingereza kufanya mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya Yemen na kuua shahidi raia 18.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema katika taaria yake kutokea Ukanda wa Ghaza, kwamba inalaani jinai hizo mpya za Uingereza na Marekani kwani ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na ni shambulio dhidi ya utulivu wa Yemen.

HAMAS imetangaza kushikamana kikamilifu na watu wa Yemen na kupongeza uungaji mkono wa taifa hilo kwa kadhia ya Palestina na mapambano yake ya ukombozi kutoka kwenye makucha katili ya utawala vamizi wa Israel, hususan katika kipindi chote cha vita vya zaidi ya miezi 15 vya mauaji ya umati yaliyofanywa na utawala katili wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Ghaza. 

Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina pia imelaani jinai hizo mpya za Marekani na Uingereza na kusema kuwa madola hayo ya kibeberu yamethibitisha bila ya aibu kuwa ni watenda jinai na wavamizi kama Israel.

Imesema, inawaunga mkono wananchi wa Yemen na Muqawama wa nchi hiyo ya Kiarabu na Kiislamu mbele ya njama na hujuma wanazofanyiwa kutokana na msimamo wao usiotetereka wa kuliunga mkono taifa la Palestina.

Nayo Kamati ya Muqawama ambayo inajumuisha pamoja makundi kadhaa ya Muqawama imelaani umwagaji damu mpya uliofanywa na Marekani na Uingereza huko Yemen ili kulilinda dola katili la Israel.

Kundi jingine la Muqawama yaani Kata’ib Hizbullah la Iraq limelaani jinai hizo mpya za Marekani na Uingereza nchini Yemen na kusema kuwa madola hayo yamethibitisha kuwa ndio wafadhili wakuu rasmi wa jinai zinazofanywa na Wazayuni kwenye eneo hili.

Mashambulizi ya Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen yalifanyika jana Jumamosi baada ya Sana'a kutekeleza marufuku ya vyombo vya Israel na kila kinachoelekea kwa utawala wa Kizayuni, kutumia Bahari ya Sham (Bahari Nyekundu) kutokana na Israel kutia ulimi puani na kutoheshimu makubaliano ya kusimamisha vita kati yake na HAMAS. Yemen inautaka utawala wa Kizayuni ufungue vivuko vya Ghaza na misaada iwafikie Wapalestina vile inavyotakiwa.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha