Kabla ya kutoa amri hiyo, Trump alishaagiza shehena za silaha na zana za kijeshi zianze kupelekwa tena Ukraine, suala ambalo kabla ya kufanyika uchaguzi wa Marekani, alilitaja kama jaribio lililokuwa likifanywa na serikali ya wakati huo ya Washington la kuanzisha na Russia Vita Vikuu vya Tatu vya Dunia.
Hivi sasa ndege za kivita za Marekani zinashambulia kwa mabomu na makombora sehemu kadhaa za ardhi ya Yemen kwa kisingizio cha kudhamini amani na usalama katika Ghuba ya Aden, Bahari Nyekundu na Mlango-Bahari wa Bab al-Mandab. Katika saa za mwanzoni tu za mashambulizi hayo makubwa, duru za tiba nchini Yemen zimeripoti kuuawa makumi ya raia.
Katika kukabiliana na uchokozi huo wa Marekani, maafisa wa serikali ya Yemen walioko mjini Sana'a wameapa kwamba, watajibu uchokozi huo wa wazi kabisa dhidi ya nchi yao kwa hatua kali kabisa zitakazo yumkinika kuchukuliwa. Operesheni ya kijeshi ya Marekani nchini Yemen bila shaka itazidi kuvuruga usalama katika eneo hilo. Wamarekani wanadai kwamba, wameanzisha mashambulizi hayo kwa lengo la kuhakikisha vyombo vya majini vinafanya safari zao kwa uhuru katika eneo hilo; hata hivyo tajiriba ya miongo miwili ya karibuni imeonyesha kuwa, kila Wamarekani walipowasha moto wa vita kwa wanachodai wenyewe kurejesha utulivu, wamevuruga zaidi hali ya usalama.
Kabla ya kuwa rais, Trump alikuwa mkosoaji mkubwa na wa kila mara wa hatua za kuzusha mivutano na zilizogharimu mno kifedha za marais waliomtangulia wa Marekani. Kwa mfano, alivielezea vita vyote vilivyoanzishwa baada ya matukio ya Septemba 11, 2001 katika eneo la Asia Magharibi kuwa ni hatua ambazo hazikuwa na tija na akasema, vita hivyo viliwagharimu walipa kodi wa Marekani dola trilioni saba. Trump alikosoa vikali pia serikali iliyotangulia ya Marekani kwa kutumia dola bilioni 350 katika vita vya Ukraine.
Lakini pamoja na hayo, kwa vile sasa hivi ameshakuwa rais wa Marekani na ameshika hatamu za Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya nchi hiyo, Trump ameitumbukiza Marekani katika vita vingine vya Yemen, ambavyo kwa kuzingatia tajiriba ya huko nyuma, havitapelekea Yemen kushindwa.
Ni takriban miaka 20 imepita tangu Marekani ilipofanya mashambulizi ya kwanza ya kijeshi dhidi ya Yemen; na kwa muda wote huo, Wayemen wamehimili na kukabiliana pia na mashambulizi makubwa ya muungano wa kijeshi ulioongozwa na Saudi Arabia. Hata hivyo, sio tu Yemen haikushindwa, lakini imezidi kuwa imara na yenye nguvu zaidi siku baada ya siku, mpaka kufikia hadi ya sasa hivi kuwa na makombora ya kisasa ya ardhini, angani na baharini ambayo yametoa changamoto kali kwa Jeshi la Wanamaji la Marekani na washirika wake.
Si hayo tu, lakini Wayemen wamefanikiwa pia kurusha makombora kadhaa yaliyolenga na kuvuruga ngome za Wazayuni katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ambayo iko umbali wa zaidi ya kilomita elfu mbili kutoka ardhi ya Yemen. Katika mazingira kama hayo, Wamarekani wanaweza kweli kushambulia kwa mabomu vituo vya kijeshi na vya kiraia vya Yemen na kuua raia wasio na hatia, lakini ni baidi kwamba wataweza kuwalazimisha Wayemen wasalimu amri.
Kwa kuzingatia hali hiyo, inaweza kutabiriwa tokea sasa kwamba mkakati wa kijeshi wa serikali ya Trump kuhusiana na Yemen utakabiliwa na hatima sawa na ya mkakati uliotekelezwa na serikali za George W. Bush, Barack Obama, Joe Biden, na hata wa serikali yake yeye mwenyewe ya muhula wa kwanza kuhusiana na nchi hiyo.
Mashambulizi hayo ya Marekani dhidi ya Yemen na kuanzishwa tena upelekaji misaada ya kijeshi ya Washington nchini Ukraine yanaonyesha kuwa kushupalia na kuwasha moto wa vita ni kimelea kinachotembea ndani ya mishipa ya damu ya sera za nje za Marekani, na wala haijalishi ni mtu gani au chama kipi nchini Marekani kinashika hatamu za urais. Alaa kulli hal, yeyote anayekalia kiti cha urais wa Marekani huwa ama anaanzisha vita, au anaendeleza vile vilivyoanzishwa, au huwasaidia wengine kupigana vita, huku raia wasio na hatia wakiendelea kuwa wahanga wa uraibu wa kuwashupalia na kuwasha moto wa vita walionao wanasiasa wa Marekani.../
342/
Your Comment