16 Machi 2025 - 18:07
Source: Parstoday
Canada kuangalia upya mkataba wa kununua ndege za kivita za Marekani

Waziri Mkuu mpya wa Canada, Mark Carney ametoa amri ya kupitiwa upya mkataba wa nchi hiyo na kampuni ya silaha ya Marekani unaohusiana na kuiuzia Canada ndege za kivita za F-35.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, hatua hiyo ya Canada imekuja baada ya rais wa Marekani Donald Trump kuziongezea ushuru bidhaa za Canada na hivyo kuzusha wimbi jipya la migogoro kati ya nchi hizo mbili jirani.

Ikiwa ni kujibu hatua za hivi karibuni za Trump, waziri mkuu wa Canada ameamuru kupitiwa upya mkataba wa nchi hiyo na kampuni ya masuala ya kijeshi ya Marekani iitwayo Lockheed Martin.

Televisheni ya Bloomberg imeripoti kwamba, Carney amemwagiza waziri wa ulinzi wa Canada kuangalia upya mpango huo ili kuona kama una manufaa kwa Canada hivi sasa au la. 

Ripoti zinaonyesha kuwa katika makubaliano ya hivi karibuni kati ya nchi hizo mbili, Canada imekubali kununua ndege 88 za kivita za F-35 kutoka kwa Marekani zenye thamani ya bilioni 19 ili kuchukua nafasi ya ndege zilizozeeka.

Kuna ushahidi kwamba baadhi ya nchi nazo pia zimeamua kuangalia upya mikataba yao na wakandarasi wa Marekani.

Donald Trump aliandika kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Truth Social, kwamba ameongeza ushuru wa forodha kwa bidhaa za chumi na alumini kutoka Canada hadi 50% na kwamba Canada inapaswa kufuta mara moja ushuru wake kwa bidhaa za Marekani hatua ambayo imejibiwa kwa hatua kali na serikali na wananchi wa Canada.

Trump amesema kuwa, Canada lazima iondoe ushuru wa asilmia 250 hadi 390 ilioziwekea bidhaa mbalimbali za maziwa za Marekani. Ametishia kuwa, kama Canada haitaondoa ushuru wake (wa kulipiza kisasi), basi kuanzia mwezi ujao (wa Aprili Trump) ataongeza ushuru wa forodha kwa magari yanayoingia Marekani kutokea Canada.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha