Taarifa iliyotolewa leo asubuhi na Vikosi vya Ulinzi vya Yemen imeeleza kwamba, vikosi hivyo vimeilenga kwa mara ya pili katika muda wa saa 24 zilizopita manowari ya kubebea ndege za kivita ya Marekani ya USS Harry Truman kwa makombora kadhaa ya balestiki na ya kruzi na ndege zisizo na rubani katika mapigano yaliyoendelea kwa saa kadhaa kaskazini mwa Bahari Nyekundu.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vimeweza kuzima mashambulizi ya kiovu ambayo adui alikuwa akijiandaa kuyafanya dhidi ya Yemen; na baada ya kurusha makombora kadhaa na ndege zisizo na rubani kuilenga manowari hiyo na manowari nyengine kadhaa, ndege zake za kivita zililazimika kurejea zilikotoka".
Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vimeendelea kueleza katika taarifa yake kwamba, operesheni ya vikosi hivyo imetekelezwa katika fremu ya kujibu uchokozi wa mtawalia wa Marekani dhidi ya Yemen na katika maadhimisho ya Vita Vikuu vya Badr, ukiwa ni muendelezo wa njia ya Uislamu katika kukabiliana na dhulma na Uistikbari.
Kwa mara nyingine tena, Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vimesisitiza kuwa kwa kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu vinaendelea kukabiliana na mashambulizi hayo ya kijinai, na kwamba iwapo makabiliano hayo yatazidi kuongezeka, watasonga mbele zaidi katika kutekeleza yale yaliyoelezwa katika hotuba ya Kiongozi wa Ansarullah, Sayyid Abdul Malik Badr al-Din al-Houthi, kuhusiana na machaguo mengi zaidi iliyonayo Yemen.
Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vimewatumia salamu za kuwatakia amani wananchi wote adhimu wa Yemen na wale wote waliokomboka kifikra katika Umma wa Kiislamu ambao wametangaza upinzani wao dhidi ya uchokozi huo wa Marekani na kusisitiza kuwa, vitaendeleza operesheni zake za kuzuia meli za utawala wa Kizayuni zisipite katika eneo hadi pale mzingiro dhidi ya Ghaza utakapoondolewa.../
342/
Your Comment