Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) - ABNA -; Imam Ali (a.s) ni Khalifa na Imam wa Kwanza katika jumla ya Maimamu 12 (amani iwe juu yao) wanaotokana na Nyumba Tukufu ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w.), na wanaofuatwa na Waislamu wa Madhehebu ya Shia Ithna Ashari.
Ama kwa upande wa Waislamu wa Madhehebu ya Sunni, wao wanamtambua kama Khalifa wa nne. Kwa maana kwamba, hata kama kuna tofauti kuwa ni Khalifa wa kwanza au wane, lakini bado kuna itifaki baina ya Shia na Sunni kuwa Imam Ali (a.s) ni Khalifa katika Makhalifa wa Mtume Muhammad (s.a.w.w): Hivyo, Mashia wanamtambua Imam Ali (a.s) kuwa ni Khalifa wao, na Masunni vile vile wanamtambua kuwa ni Khalifa wao.
Imam Ali (a.s) ni Mtu wa Kwanza kuzaliwa ndani ya Msikiti na Kuuliwa ndani ya Msikiti
Imam Ali (a.s) anazo sifa na fadhila kemkem. Katika sehemu hii tutataja sehemu ya sifa na fadhila zake, nayo ni hii kuwa: Imam Ali (a.s) alikuwa ndiye mtu wa kwanza kuzaliwa ndani ya Al-kaaba ambayo kila Muislamu anatambua kuwa Al-Kaaba ni Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu (s.w.t). Pia aliuliwa Kishahidi akiwa ndani ya Msikiti wa Al-Kufa. Kwa mantiki hiyo, Imam Ali (a.s) mwanzo wa uhai wake ulikuwa ni Msikitini na mwisho wa uhai wake vile vile ulikuwa ni Msikitini!.
Imam huyu na Kiongozi wa Waumini (amani iwe juu yake) alizaliwa Siku ya Ijumaa (tarehe 13, Rajab, Mwaka wa 30, maarufu kama Mwaka wa Tembo (600 A.D) akiwa katika hali ya kusujudu, akimsujudia Allah (s.w.t) ndani ya Nyumba Tukufu ya Allah (s.w.t) huko Makka, na Allah alimbariki mwisho mwema kwa kuuliwa kishahidi alfajiri ya siku ya Ijumaa, huku akiwa amesujudi vile akimsujudia Allah (s.w.t) ndani ya Msikiti wa Al-Kufa. Hii ni fadhila ya kipekee kwake, kiasi kwamba hakuna Mwanadamu aliyewahi kuipata fadhila hii na hatoipata kamwe mtu mwingine baada yake.
Mwandishi Mashuhuri Abbas Mahmud Aqaad amelibainisha hilo kwa kauli yake: “Imam Ali alikuja duniani hali ya kuwa paji lake la uso wake likiwa limeandikwa Shahada, na alitoka katika dunia ikiwa Shahada imeandikwa juu ya paji lake la uso kwa pigo la (upanga wenye) sumu, na kwa ujumla hilo halina ubishi, na halihitaji mpigaji picha wala mchunguzaji, kwani picha hiyo ya mpiganaji katika njia ya Mwenyezi Mungu ilikuwapo mkononi mwake, moyoni mwake na akilini mwake, au ni sura ya mwenye kufa kwa ajili ya kutetea dini”.
Kisha anasema: Hakika alizaliwa kama tulivyojua ndani ya al-Kaaba, na kupigwa upanga ndani ya Msikiti, hiyo ni alama ya kufafana kwa uhai wake, mwanzo wake na mwisho wake”. (Rejea: Abqariyyat Imam Ali (a.s), uk. 155-156, cha Abbas Mahmud Aqaad).
Kwa mujibu wa ukweli huu, tunatambua pasina shaka yoyote kuwa uhai wake wote ulikuwa ni kwa ajili ya Dini Tukufu ya Kiislamu, pia ujumbe wake maishani mwake ulikuwa ni kazi ya kuhudumia Uislamu na Waislamu, na kutetea itikadi na imani sahihi ya Kiislamu.
Ushujaa wa Imam Ali (a.s) hauna kifani
Moja ya matukio ya ushujaa na ujasiri wa Imam Ali (amani iwe juu yake), ilikuwa ni kulala kwake katika Kitanda cha Mtume Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake na Aali zake) ili kuokoa Maisha yake, akajitolea yeye mhanga na kuitanguliza nafsi yake katika hatari, maadam ana uhakika na anatambua kuwa kwa kufanya vile atahakikisha anaunusuru uhai wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Aidha, Maisha yake yote yalikuwa ni Maisha ya kuweka uthabiti na kuimarisha nguzo na misingi ya Uislamu, pia kujitolea muhanga kwa kitu ghali na chenye thamani kubwa, ili kuhakikisha neno la Mwenyezi Mungu linakuwa juu, na neno la makafiri linakuwa chini.
Na hiyo ni sehemu nyingi ya Fadhila ya Imam Ali (a.s), inayotambulika kama Fadhila ya kupigana Jihadi na kujitolea muhanga kwa ajili ya kuuhami Uhai wa Uislamu na Uhai wa Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w), kiasi kwamba mpaka akata sharafu kubwa na lakabu ya kuitwa Simba wa Mwenyezi Mungu mwenye kushinda. Vita ngumu na iliyoshindikana ilikuwa ni vita nyepesi kwake, masahaba wote watashindwa kurudi na ushindi katika vita hiyo, lakini akienda yeye Amirul Muuminin (a.s), lazima arudi na ushindi. Na sifa hii ya ushujaa vitani inapatikana kwa wachache mno miongoni mwa Masahaba wa Mtume (s.a.w.w), na kinara wao ni Amirul-Muuminina Ali bin Abi Twalib (a.s).
Your Comment