Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Kimataifa la Ahl al-Bayt (AS) - Abna -; Idadi ya Mashahidi wa vita vya mauaji ya halaiki vilivyoanza tarehe 7 Oktoba 2023 na wavamizi wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza imefikia zaidi ya Mashahidi elfu 50. Wengi wa Mashahidi hao ni watoto na wanawake, na wakati huo huo, maelfu ya watu wengine ni miongoni mwa waliopotea.
Kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza, katika takwimu zilizochapishwa hivi punde zaidi, katika saa 24 zilizopita, Mashahidi 41 na Majeruhi 61 wamehamishiwa katika Hospitali za Ukanda wa Gaza. Takwimu hii inaongeza jumla ya idadi ya Mashahidi wa vita tangu Machi 18, 2025 hadi Mashahidi 673 na 1,233 waliojeruhiwa. Baada ya kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano, uvamizi wa Israel kwa mara nyingine umeendeleza mauaji ya kimbari katika eneo hili.
Wizara ya Afya ilitangaza kuwa, jumla ya Mashahidi wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni tangu tarehe 7 Oktoba 2023 imefikia watu 50,021 na idadi ya waliojeruhiwa imefikia watu 113,274.
Wakati wa mauaji hayo ya kimbari, wavamizi wa Israel wamefanya mamia ya jinai dhidi ya raia katika Ukanda wa Gaza, ambao umezingirwa kwa zaidi ya miaka 17. Uhalifu huu umeua makumi na mamia ya watu kila siku tangu kuanza kwa vita hadi sasa.
Vikosi vya Israel vilivyovamia kwa mabavu vilishambulia makazi ya wakimbizi hao ambao walikuwa wamekusanyika katika hospitali na shule na kushambulia maeneo ambayo hapo awali yalitangazwa kuwa "salama". Hatua hizi ziliua idadi kubwa ya watu waliokuwa wakijaribu kutoroka mashambulizi hayo ya anga.
Idadi kubwa zaidi ya Mashahidi wa vita hivi ilitokana na milipuko ya mabomu kutokana na mashambulizi ya ndege za anga. Kwa kuungwa mkono na Marekani, Israel imetumia makumi ya maelfu ya tani za vilipuzi kushambulia Ukanda wa Gaza. Mashambulio haya ya mabomu yameharibu vituo vya wakimbizi na nyumba za raia ambazo zilikuwa zimejaa watu waliokimbia makazi yao.
Mnamo Januari 19, makubaliano ya kusitisha mapigano yalipoanza kutekelezwa kupitia upatanishi wa Qatar, Misri na Marekani, mashambulizi ya mabomu katika Ukanda wa Gaza yalipunguzwa kwa muda mfupi. Makubaliano hayo yalitakiwa kutekelezwa kwa awamu tatu ili kupelekea usitishaji vita wa kudumu, lakini wavamizi wa Israel walikaidi makubaliano hayo baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza.
Vita hivyo vilianza tena Jumanne iliyopita asubuhi, na wakati huo huo, mamia ya mashambulizi makali ya anga yalifanyika katika Ukanda wa Gaza, ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 400, wakiwemo karibu watoto 200, ndani ya saa chache.
Kuanza tena kwa vita kulikuja kama mshtuko mkubwa kwa wakaazi wa Gaza, ambao walikuwa wakijaribu kurejea katika kiwango cha chini kabisa cha maisha ya kawaida wakati wa kipindi cha usitishaji vita. Hali hii imetokea si tu kwa sababu ya uharibifu mkubwa, bali pia kwa sababu ya kusitishwa kwa misaada katika wiki za hivi karibuni kutokana na kufungwa kwa vivuko vya mpaka na utawala wa Kizayuni.
Mbali na mashambulizi ya angani, jeshi linaloikalia kwa mabavu (Palestina) la Israel limepenya tena maeneo ya ardhini ambayo yaliondolewa kutoka kwao kwa mujibu wa makubaliano. Katika siku za hivi karibuni, wavamizi hao wamewataka wakaazi wa maeneo kadhaa kuyahama maeneo hayo, ambapo eneo la hivi punde lilikuwa ni kitongoji cha Tal Sultan huko Rafah, Kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Your Comment