Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) - ABNA - Kubomolewa Makaburi ya Baqi'i (Kiarabu: هدم قبور أئمة البقيع) kunaashiria tukio ambalo lilijiri baada ya mji wa Madina kuzingirwa mwaka 1344 Hijria. Historia inaonyesha kuwa, katika tukio hilo la kusikitisha, lililotokea tarehe 8 Mfunguo Mosi Shawwal 1345 Hijria (1925 Miladia) Mawahabi wa Saudi Arabia walibomoa makaburi ya Ahlul-Bayt -a.s- wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambayo yanapatikana katika ardhi ya Baqi’i, katika Mji Mtakatifu wa Madina.
(Jannat al-Baqi katika miaka ya 1910, kabla ya kubomolewa mara ya pili na Mawahhabi)
Baada ya Muhammad Ibn Saud kutawala tena maeneo ya Hijaz, likiwemo eneo la Madina, Sheikh Abdullah bin Bulaihad mmoja wa makadhi wa Mawahabi, alitoa fat'wa ya kuhalalisha kuharibiwa kwa makaburi matukufu na ya kihistoria ya mjini Madina. Mawahabi walikusanya watu kwa nguvu na kuwalazimisha kwenda katika makaburi hayo ya Baqi’i na kuanza kubomoa na kuharibu kila kitu kilichokuwa juu ya makaburi ya mji wa Madina na nje ya mji huo.
Miongoni mwa makaburi yaliyobomolewa na kuharibiwa vibaya ni makaburi manne ya Maimamu na wajukuu wa mtukufu Mtume (s.a.w.w) ambao ni Imamu Hassan (a.s), Imamu Sajjad (a.s), Imamu Baqir (a.s) na Imamu Swadiq (a.s). Makaburi ya Abdullah na Amina, wazazi wa mtukufu wa Mtume (s.a.w.w), kaburi la Ibrahim mtoto wa kiume wa Mtume (s.a.w.w) na kaburi la Ummul Banin mama wa Abul Fadhlil-Abbas nayo yalibomolewa. Kaburi pekee lililobakishwa na Mawahabi hao ni la mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w), kwani walijua kuwa kubomoa kaburi la mtukufu huyo kungezua hasira kali za Waislamu duniani.
Mawahabi mara mbili, awali ilikuwa 1220 Hijria na 1344 Hijria wakitegemea fat'wa za Mamufti 15 wa Madina zinazosisitiza kwa kauli moja juu ya marufuku ya kujenga jengo juu ya makaburi na ulazima wa kulibomoa, walibomoa maeneo na majengo yaliyokuwa yamejengwa katika makaburi ya Baqi'i. Kubomolewa makaburi hayo kulikabiliwa na radiamali ya watu na Maulamaa wengi nchini Iran, Iraq, Pakistan, Muungano wa Kisovieti na kadhalika.
(Video Fupi / Bonyeza picha hiyo hapo juu utizame eneo hilo la Jannatul-Baqii)
Serikali ya wakati huo ya Iran katika radiamali yake dhidi ya kubomolewa maeneo matakatifu ya Waislamu ilitangaza siku moja ya maombolezo ya kitaifa na kufuatilia tukio hilo, ikaakhirisha kwa miaka mitatu kuitambua rasmi nchi ya Saudi Arabia iliyokuwa ndio kwanza imeasisiwa.
Baada ya makaburi ya Baqi'i kubomolewa eneo hilo likawa ni ardhi ya tambarare. Hata hivyo, sehemu yalipo makaburi ya Maimamu wanne imewekewa alama ya mawe na hivyo yanatambulika. Juhudi za Maulamaa wa Kishia na vilevile serikali ya Iran za kuhakikikisha juu ya makaburi ya Maimamu hao wanne kunawekwa kivuli na vilevile kujengewa ukuta kuzunguka makaburi hayo hazijazaa matunda licha ya serikali ya Saudia kuafiki hilo katika hatua ya awali.
Maulamaa wa Kishia mbali na kulalamikia kubomolewa makaburi ya Baqi’i na kusawazishwa na ardhi, wametunga na kuandika vitabu kuhusiana na misingi ya Uwahabi na kubomoa kwao maeneo matakatifuu.
Miongoni mwa vitabu hivyo ni Kashf al-Irtiyab kiilichoandikwa na Sayyid Muhsin Amin na Da'wat al-Huda kilichoandaikwa na Muhammad Jawad Balaghi. Inaelezwa kuwa, Mawahabi lilikuwa kundi la kwanza kubomoa maeneo ya kidini likitegemea mitazamo na nadharia ya kidini.
Your Comment