7 Aprili 2025 - 22:59
Source: Parstoday
Wanaharakati Iran watangaza kuwa tayari kupambana na Marekani

Wanaharakati zaidi ya 300 wa jumuiya za kiraia nchini Iran wamepinga vikali vitisho vya Marekani vya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya nchi yao, wakiapa kukabaliana na uvamizi wowote wa kigeni.

Katika taarifa yao kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, wanaharakati hao, wakiwemo maprofesa wa vyuo vikuu, wataalamu wa sheria, watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari na wanaharakati huru wa kisiasa, wamesisitiza dhamira yao ya kulinda Iran licha ya tofauti zao na serikali.

Wamesema: “Licha ya mitazamo tofauti na serikali, sisi – tunaotia saini taarifa hii – tutaipigania nchi yetu kwa nguvu zote endapo kutakuwa na mashambulizi dhidi ya Iran. Tutapigana kwa ajili ya Iran, ubinadamu na amani ya dunia.”

Wameongeza kuwa shambulizi lolote dhidi ya Iran halihusu serikali pekee, bali litawalenga wananchi wa Iran na kuhatarisha utulivu wa ukanda mzima.

Wanaharakati hao pia wameitaka jamii ya kimataifa kuchukua msimamo thabiti dhidi ya uhalifu wa utawala wa Israeli na vitisho vya kivita vya utawala mpya wa Marekani. Wamesema sera za Rais Donald Trump za kutegemea mabomu na vita, zinakiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kuiibua tishio kwa amani ya kimataifa.

Aidha wamepinga uingiliaji wa ajinabi katika masuala ya kisiasa nchini Iran. Halikadhalika wameashiria uingiliaji wa madola ajinabi katika masuala ya eneo la Magharibi mwa Asia wakitoa mfano wa vita vya kulazimishwa vya miaka ya 1980,  na kuelezea jinsi madola ya Mashariki na Magharibi yalivyomuunga mkono Saddam katika uvamizi wake dhidi ya Iran.

Wanaharakati hao wamehitimisha kwa kuonya sera za upendeleo za Magharibi, zinazopuuza silaha za nyuklia za utawala wa Kizayuni wa Israel huku zikilenga mpango wa nyuklia wa Iran ambao ni wa amani na ulio chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha