Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul Bayt (A.S) - Abna - , Mikutano kati ya ujumbe wa harakati ya Hamas na maafisa wa Misri Mjini Cairo imeongezeka kwa kasi. Kwa wakati huu, vuguvugu la Hamas limeonyesha "kubadilika" kwake kuelekea pendekezo lililorekebishwa la Misri la kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza. Pendekezo hilo linajumuisha kusitishwa kwa mapigano kwa siku 40-70, ambapo kumetakiwa kuachiliwa huru wafungwa wanane hai wa Israel na kukabidhi miili ya wengine wanane.
Kwa kubadilishana na kuachiliwa kwa watu hao, idadi ya wafungwa wa Kipalestina katika magereza ya Israel ambayo Misri imedai kuachiliwa kwao inakadiriwa kuwa karibu 1,100. Kati ya hawa, kundi miongoni mwao litahamishiwa Misri na nchi nyingine, na makubaliano hayo pia yatajumuisha kuachiliwa kwa mfungwa wa Kimarekani Aidan Alexander. Walakini, Tel Aviv inaendelea na ujanja wake wa kuelezea muafaka wake thabiti juu ya makubaliano haya.
Kwa mujibu wa afisa mmoja wa Misri, makubaliano yanayojadiliwa yanaweza kusababisha kuachiliwa kwa wafungwa 11 wa Israel na kukabidhiwa miili 16 ikiwa watafikia usitishaji mapigano wa siku 70. Hii inaweza kufungua njia kwa usitishaji mapigano kuendelea hadi baada ya Eid al-Adha, na pamoja na hayo, kuwasili kwa wingi kwa misaada ya kibinadamu kila siku, kulingana na mifumo ya makubaliano ya hapo awali.
Pendekezo hilo la Misri linajumuisha kuondoka kwa Israel kutoka maeneo kadhaa ambayo yamekuwa yakikaliwa kwa mabavu katika siku za hivi karibuni na kutoa vifaa vya kuhama ndani ya Gaza. Wakati huo huo, kuna vitisho vya Israel vya kuzidisha operesheni za kijeshi ikiwa usitishaji mapigano hautatiwa saini haraka, jambo ambalo Cairo inaona kama "jaribio la shinikizo la dakika za mwisho ili kupata makubaliano zaidi."
Duru za habari zinasema kuwa Hamas imejibu vyema mapendekezo ya mamlaka ya Misri, ikisisitiza haja ya kuharakisha uokoaji wa hali mbaya ya kiafya huko Gaza na kuondolewa kwa mzingiro ambao sasa unawalenga raia wote bila kubagua. Pande hizo mbili pia zilijadili "kuundwa kwa kamati ya uratibu kwa ajili ya usimamizi wa Gaza katika kipindi cha mpito cha miezi sita," ndani ya mfumo wa mpango wa Misri wa kurejesha umoja wa Ukingo wa Magharibi na Gaza chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Palestina.
Your Comment