9 Aprili 2025 - 14:10
Maisha kwa mtindo wa Wahyi: Je! Qur'an Inatuonyeshaje Njia ya Maisha ya Furaha (Saada)?

Kuelewa mtindo wa maisha katika zama za sasa, ambazo ni zama za Ghaiba, ni swali muhimu. Kwa sababu kazi muhimu ni kuelimisha kizazi kinacholingana na zama za wahyi ili kumsaidia Imamu wa Zama (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake na faraja yake). Kwa kuzichunguza kwa makini Aya na riwaya, kudhihiri na kuonekana kwa maisha mazuri na hatimaye kufikia maisha sahihi katika kipindi cha kudhihiri, kutadhihirika katika mwanga au kivuli cha elimu na marifa juu ya Hojja wa Mwenyezi Mungu.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul Bayt (a.s) - ABNA - Maisha ya kawaida ya Binadamu daima yameambatana na mashinikizo ambayo Wanadamu huyasababisha wao wenyewe. Wanadamu wote, katika hali yoyote ile waliyo nayo, wanatamani maisha ya raha na kuwa na maisha mazuri na ya kawaida yasiyo na wasiwasi, misukosuko na mahangaiko yoyote ndani yake. Lakini uhakika ni kwamba maisha ya Mwanadamu huambatana na mahangaiko, mshuko-moyo, misukosuko, na mifadhaiko, na hayo yamekuwa sababu ya kuwatenganisha Wanadamu na kusudi la maisha.

Maisha, kwa upande wake, ni kama fumbo gumu na tata; Sasa, ikiwa Wanadamu wenyewe wataongeza utata na ugumu huu, basi kwa hakika hakuna kitakachobaki. Kawaida, katika maisha yote (ya Mwanadamu), watu hufikiria kila wakati juu ya kesho au makosa waliyofanya zamani (kwa maana, muda wote wanashughulishwa na yaliyopita katika wakati uliopita waliouishi), na hawajaribu au hawafanyi jitihada za kuishi sasa (au jitihada za kuuishi wakati uliopo). Suala hili ni mwanzo wa wasiwasi na huzuni katika maisha (yao).

Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu Alayhi wa Aalihi wa Sallam) anasema:

(اِذَا التَبَسَت عَلَیکُمُ الفِتَنُ، کَقِطَعِ الَّیلِ المُظلِمِ فَعَلَیکُم بِالقُرآنِ)

 "Inapokufunika mitihani, kama usiku wa giza, ni juu yako kushikamana na Qur'an." [1]

Kwa ibara  nyingine, maana ya riwaya hii ni hii kwamba: Wakati wowote pindi majaribu yatakapokufunikeni kama vile usiku wa giza, na kukufanyeni muwe na shaka, wasi wasi (na mifadhaiko), basi irejeeni / shikamaneni na Qur'an. Na "Majaribu" maana yake ni yale yanayosababisha uwe na wasiwasi, kuchanganyikiwa au kukanganywa na kuvurugika akili, mawazo na hali yako, na kuleta ile hali ya mfadhaiko na kutoelewa au kutambua lolote ndani ya mtu, na kusababisha shinikizo kwenye nafsi, akili na mwili wa mtu (kwa maana: Kumletea mtu tatizo la kisaikolojia au ugonjwa wa kisaikolojia).

Riwaya hii ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu Alayhi wa Aalihi wa Sallam) inamuongoza Mwanadamu kutafuta hifadhi ya Qur'an pale anapokabiliwa (au anapovamiwa) na Mitihani (Majaribu) na matatizo (maishani mwake).

Maisha kwa mtindo wa Wahyi: Je! Qur'an Inatuonyeshaje Njia ya Furaha (Saada)?

Qur'an ni maneno bora zaidi, kwa sababu ni Maneno Matukufu ya Mwenyezi Mungu na yanatokana na elimu na uwezo Wake usio na kikomo wala mipaka. Kwa hivyo, ni lazima tuone ni suluhisho gani Qur'an Tukufu imetoa kwa ajili ya kushinda matatizo haya ili tuweze kufikia mtindo wa maisha bora wa Qur'an. Qur'an ambayo kwa mujibu wa Imam Ali (amani iwe juu yake) ni wema (au) ihsani isiyosaliti kamwe, [2], - (kwa maana Quran inamtakia mja maisha ya kheri na wema, na inamuongoza katika hayo na haiwezi kamwe kumsaliti katika kumtakia kheri na maisha mazuri, hivyo) - imependekeza fikra na mtindo maalum kwa ajili ya maisha ya Mwanadamu, ikiyaita maisha hayo kuwa ni Maisha Mazuri (حَيَوٰةً طَيِّبَةً)

مَنْ عَمِلَ صَٰلِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُۥ حَيَوٰةً طَيِّبَةً ۖ وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُواْ يَعْمَلُونَ -  ili kupitia kwayo mtu aweze kufikia daraja au hali ya kuwa karibu na Mwenyezi Mungu na katika dhihirisho la Sifa za Mwenyezi Mungu. Bila kusahau kwamba: Katika Aya hii Tukufu, imetajwa Imani kama sharti la uhalali (kuswihi) na kukubalika kwa matendo mema. Kwa maana, matendo hayataitwa au hayaitwi matendo mema ila kwa imani, hivyo ni lazima imani iwepo na kisha utende matendo mema, malipo yake ni Mwenyezi Mungu kukuhisha kwa Maisha Mazuri au kukufanya uishi Maisha yaliyokuwa mazuri. Na kuishi Maisha Mazuri hapa Duniani kuna maana pana sana, ni pamoja na kuishi maisha yanayokuelekeza katika njia ya Peponi na kukuepusha na njia ya kuelekea katika Moto wa Jahannam.

Imepokewa kutoka kwa Imamu Sadiq (a.s) - katika mwendelezo wa riwaya iliyotangulia hapo juu - anasema kwamba Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w) amesema [3]:

«مَنْ جَعَلَهُ أمَامَهُ قَادَهُ إلَى الْجَنَّة»

"Yeyote atakayefanya harakati zake kwa kuifuata Qur'an, itamuongoza na kumpeleka Peponi".

 «وَ مَنْ جَعَلَهُ خَلْفَهُ سَاقَهُ إلَى النَّار»

"Na atakaye chagua njia isiyokuwa ya Qur'an, basi njia hiyo itamkokota na kumfikisha Motoni".

«هُوَ الدَّلِیلُ عَلَى خَیْرِ سَبِیل»

Ni muongozaji kuelekea njia iliyokuwa bora.

Maisha Mazuri

Qur'an inatuelekeza mambo mengi ya kufanya na kutokufanya maishani mwetu, na kuyazingatia mambo hayo katika maisha yetu, ni mojawapo ya sababu zinazotengeneza mtindo wa maisha wa mtu. Makala hii fupi haina lengo la kuchunguza kila moja ya mambo haya yanayotakiwa kufanywa na yale yasiyotakiwa kufanywa. Hivyo inatosha kusema hapa kwamba Qur'an inazingatia mtindo maalum wa maisha, na kwamba mtindo maalum wa maisha unaweza kupatikana kutokana na jumla ya mijadala ya Qur'an ya kimafundisho, kimaadili, kihukumu za Qur'an, kihistoria, ibada, amri na makatazo.

-

Rejea:

[1] Al-Kafi (toleo la Kiislamu), Juz. 2, uk. 598 Wasa’il al-Shi’a, Juz. 6, uk. 171 Bihar al-Anwar (chapa ya Beirut), Juz. 74, uk. 134.

[2] Imam Ali (a.s), Nahjul-Balaghah.

[3] Al-Kafi (toleo la Kiislamu), Juz. 2, uk. 598 Wasa’il al-Shi’a, Juz. 6, uk. 171 Bihar al-Anwar (chapa ya Beirut), Juz. 74, uk. 134.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha