Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Neno “Hijab” ni neno la Kiarabu lenye maana ya kusitiri (au stara), pazia, baibui, mtandio, au ushungi. Neno hili limetumika katika Qur'an Tukufu kwa maana ya kuwatenga (kuwawekea pazia) Wanawake kutokana na Wanaume wanaoweza kuoana nao, lakini hawakuoana nao au hawajaoana nao bado, kwa maana: (Wanaume ambao ni Ghair-Mahram wao - Yaani: Wanaume ambao sio haram kwao kuwaoa Wanawake hao).
Hivyo, kwa Wanawake wa Kiislamu, kutochanganyika na Wanaume ajnabi au wageni kwao (kwa maana: Wanaume ambao wanaweza kuwaoa kisheria / sio haram kwao kuwaoa) na kuvaa baibui au ushungi au mtandio au stara watokapo nje ya nyumba zao, ni amri ya Mwenyezi Mungu, wala si kwa ajili ya lolote lile miongoni mwa yale wanayoyafikiria wale wajinga, au yale wanayoyasema maadui wa Uislamu; kama tutakavyoona katika hotuba hii fupi.
Hotuba hii ilitolewa na Sayyid Sa'eed Akhtar Rizvi katika Semina ya nane ya "Golden Crescent Group" iliyofanyika Mjini Lushoto, mnamo tarehe 22 /10/ 1977.
Kiini cha Uislamu ni "Kujitoa kabisa ili kutimiza Penzi la Mwenyezi Mungu", kuzifanya fikra na mwelekeo wa mtu kuwa wenye kuzitii Amri za Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) Anasema:
"Haiwi kwa Mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri, wawe na hiari katika shauri lao; Na mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika amepotea upotevu ulio wazi." (Qur’ani, 33:36).
Hivyo basi, kama utauliza ni kwa nini Hijab ni wajibu, jibu pekee liwezalo kutolewa ni hili kwamba: Kwa sababu Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wameamua hivyo. Na ni lazima huo uwe mwisho wa hoja zote kwa kadiri Mwanamume aliyeamini na Mwanamke aliyeamini wahusikavyo.
Katika zama hizi, Hijabu imelinganishwa na kutoendelea kwa jamii na inafikiriwa kuwa ni ishara ya kifungo cha wanawake. Wahubiri wengi wanafikiria kuwa ni bora kutolizungumzia jambo hili katika majlisi zao. Lakini Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Inapotokea Bid’ah na Mwanachuoni asikiseme kile akijuacho (dhidi ya Bid’ah hiyo), basi (Mwanachuoni huyo) hulaaniwa na Mwenyezi Mungu, Malaika na Wanadamu.”
Islamu ni dini thabiti ambayo ndani yake sheria zote na taratibu zote vimerekebishwa vizuri na kama mtu anataka kugeuza sehemu fulani, utaratibu wote utaharibika. Ni lazima uukubali muundo mzima kama ulivyo. Huwezi kuchagua la kuchukua na la kuacha kutoka katika muundo huu.
Uislamu unaamini kuwatenganisha wanaume na wanawake.
Umewapa wanaume na wanawake madaraka tofauti kabisa, kutegemeana na uwezo wao wa kimaumbilee Mwanaume anawajibika kutafuta mahitaji ya maisha kwa ajili yake na jamii yake. Mwanamke amepewa madaraka ya kusimamia mambo ya nyumbani, na kulea watoto chini ya misingi ya Kislamu.
Watetezi wa uhuru wa wanawake huudhihaki mgawanyo huu wa kazi, wakidai kuwa malezi mazuri ya watoto ni kazi duni yenye kuwashusha cheo wanawake. Hawatambui kuwa mpango wao mpya wa kijamii, unaowanyima watoto malezi na uangalizi wa wazazi ndio sababu kubwa ya kuongezeka kwa makosa ya watoto, jambo ambalo baadaye huipasua pasua jamii.
Hijaab, kama tuijuavyo, haikuwepo Uarabuni kabla ya Uislamu. Ilianzishwa na Mtume (s.a.w.w.) mjini Madina baada ya kuteremshwa amri maalum za Qur’ani Tukufu, miaka mingi kabla ya kusilimu kwa watu wasio Waarabu.
Ummul-Mu’uminiin, Bibi Aisha alikuwa kila mara akiwasifu Wanawake wa Kiansar (wa Madina) kwa maneno haya "Baraka za Mwenyezi Mungu ziwashukie Wanawake wa Kiansar". Mara baada ya kuteremshwa Aya za Sura ya An-Nur waliacha kutoka nje (ya nyumba zao) kama walivyokuwa wakifanya kabla ya hapo. Walianza kuvifunika vichwa vyao kwa nguo nyeusi, kana kwamba kunguru alitua vichwani mwao."
Hadithi nyingine yenye maana hii hii imepokewa kutoka kwa Ummul-Mu’uminiin, Bibi Ummu Salma.
Hivyo basi, jitihada za baadhi ya Makafiri waliojifanya kuwa ni wajuzi sana wa Uislamu ya kuonyesha kuwa Hijaab iliuingia Uislamu Waarabu walipoziteka nchi jirani, hazina maana hata kidogo. Haya ni mojawapo ya misingi ya sheria za Kiislamu. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: "Kuwa na haya ndio Uislamu."
Hizi ni aina moja wapo za Hijab - aina zote hizi ni kiujumla ni stara kwa Mwanamke.Kwa maana, Hijab katika picha hiyo inasimama kama stara, Khimar ni stara, Shayla ni stara, Niqab ni Stara, Burqa ni stara, Chadori (Mara nyingi huvaliwa nchini Iran, ni stara, Abaya ni stara. Kwa hiyo, ikisemwa kuvaa hijab kwa mwanamke maana yake ni kujistiri kwake katika mavazi yake kuanzia kichwa chake shingo yake, mabega yake, na mwili mzima kwa ujumla. Kwa hiyo, Mwanamke baada ya kuvaa nguo ya kustiri mwili wake, anaweza kwa upande wa juu kuvaa Hijab au Niqab au Burqa au Chadori au Abaya au Khimar au Shayla, vyote hivyo nilivyo vitaja vinafunika nywele shingo na mabega, ambavyo ndio vitu vya wajibu kwa mwanamke kufunika, ama sura yake sio wajibu kuifunika, na sio haram akifunika pindi atakapoamua kuvaa Burqa inayofunika moja kwa moja sura yake, au akaamua kuacha sehemu ya macho atakapovaa Niqab, au kuacha sura yake wazi atakapoamua kuvaa Hijab kama inavyoonekana hapo katika picha.
Kiujumla hiyo, namna hizo hizo 7 katika picha hii, ni mitindo tu uvaaji na namna ya kujistiri, kwa mantiki hiyo, kilichokuwa muhimu na wajibu kwa Mwanamke ni hiyo Hijab kama unavyoona hapo katika picha hii kwenye taswira ya Mwanamke wa pili namna alivyo vaa Hijab yake, juu katika mstari wa kwanza.
Your Comment