22 Aprili 2025 - 22:52
Source: Parstoday
Kitendawili... Papa ajaye atatoka Afrika au Asia?

Kifo cha kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis kimeilazimisha Vatican kuitisha kongamano la kihistoria la kumchagua mrithi wake; lakini swali linaloulizwa ni kwamba, je, papa ajaye atatoka Afrika au Asia?

Ni baada ya Vatican kutangaza jana kwamba Papa Francis, ambaye jina lake halisi ni Jorge Mario Bergoglio, amefariki dunia baada ya kulazwa hospitalini kwa ugonjwa wa kupumua wa nimonia ya pande zote mbili (bilateral pneumonia). Alichukua wadhifa huo wa kuwa papa wa Kanisa Katoliki mwaka 2013 akiwa papa wa kwanza asiye Mzungu wa Ulaya, tangu karne ya 8.

Uchaguzi wa mrithi wake utafanywa na Jumuiya ya Makardinali, inayoundwa na makadinali 138 walio chini ya umri wa miaka 80 (110 walioteuliwa na Francis). Mchakato huo unaoanza wiki mbili hadi tatu baada ya kifo cha papa unahusisha upigaji kura wa siri katika Kanisa la Sistine Chapel huko Vatican. Mgombea lazima awe mwanamume Mkatoliki aliyebatizwa, lakini kwa kawaida huchaguliwa kutoka miongoni mwa makadinali. Theluthi mbili za kura zinahitajika kwa ajili ya kuchaguliwa kuwa papa, na moshi mweupe kutoka kwenye bomba la moshi la Sistine Chapel huwa ni ishara ya mafanikio ya mchakato huo.

Kuwepo makadinali wa mbari na mataifa tofauti walioteuliwa na Papa Francis kumeibua uwezekano wa kuchaguliwa papa kutoka Afrika au Asia, ikiwa ni kwa mara ya kwanza baada ya karne nyingi. Kutoka Afrika, Peter Turkson wa Ghana, aliyehudumu katika Baraza la Kipapa la Haki na Amani, na Fridolin Ambongo Besungu wa Kongo, kwa sababu ya juhudi zake za kuimarisha amani, wanatambuliwa kuwa machaguo yenye nafasi nzuri zaidi. Wote wawili ni wahafidhina na wamekuwa na ushawishi katika nchi zao.

Na kutoka Asia, Luis Antonio Tagle wa Ufilipino, kutokana na kufanana kwake na Papa Francis katika msisitizo wake juu ya haki za kijamii, ana nafasi kubwa ya kuwa papa wa kwanza Muasia.

Wengine wanaotajwa katika uwanja huu ni Peter Ordó wa Hungary na Pietro Parolin, mwanadiplomasia mkuu wa Vatican, wanatambuliwa kuwa wagombea wakuu.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha