Ni siku 50 zimepita tangu utawala wa Kizayuni uzuie kikamilifu kuingizwa misaada ya chakula, dawa na vifaa vingine muhimu katika eneo hilo la Palestina lililoharibiwa vibaya sana na vita vya kinyama vya jeshi la utawala huo, licha ya mashirika ya misaada kuonya mara kadhaa kwamba baa kubwa la njaa limesambaa huko Ukanda wa Ghaza.
Katika matamshi aliyotoa kupitia mkanda wa video alioweka kwenye akaunti yake ya X siku ya Jumatatu, Michael Huckabee, balozi wa Marekani mjini Tel Aviv alisema, Hanan Balky, mkurugenzi wa WHO wa eneo la Mashariki ya Mediterania amemhimiza aishinikize Israel iruhusu misaada ya kibinadamu kuingizwa Ghaza.
Badala ya kufanya hivyo, Huckabee amesema harakati ya Muqawama ya Palestina Hamas inapaswa kwanza iwaachilie mateka 60 wa Israel, kisha ndipo Wapalestina wa Ghaza wataweza kupokea misaada hiyo ya kibinadamu inayohitajika sana, na hivyo kutoa hitimisho kwamba si Israel bali ni Hamas ndiyo inayopasa kuwekewa mashinikizo.
Kufuatia matamshi hayo ya Huckabee, Francesca Albanese, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa amejibu kwa kumkumbusha balozi huyo wa Marekani mjini Tel Aviv kwa kumwambia: "Kifungu cha 8(2)(b)(25) cha Mkataba wa Roma, kinasema kunyima misaada ya kibinadamu ni uhalifu wa kivita."
Albanese ameendelea kueleza: "hatua hii itazidi kuifanya iwe mbaya zaidi hali ya maisha inayoteketeza jamii ya Wapalestina wa Ghaza. Hakuna anayefaidika na hili - si Wapalestina, si Waisraeli, si Waamerika wa Kaskazini - si yeyote kati yetu. Kwa pamoja, tunaweza kukomesha unyama huu".
Katika jibu lake hilo kwa balozi huyo wa Marekani katika utawala wa Kizayuni wa Israel, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa ameambatanisha pia ibara inayoashiria adhabu inayotolewa "kwa kutumia kama mbinu ya kivita kuwaweka na njaa makusudi raia kwa kuwanyima vitu vya lazima kwa maisha yao, pamoja na kuzuia kwa makusudi misaada kama ilivyoainishwa chini ya Makubaliano ya Geneva".../
342/
Your Comment