23 Aprili 2025 - 19:56
Je, Mazungumzo Kati ya Mwanamume na Mwanamke Wasiokuwa Mahramu Yamekatazwa kwa namna yoyote ile katika Uislamu?

“Kauli yenye nguvu zaidi ni hii kwamba kusikia (kusikiliza) sauti ya Mwanamke asiyekuwa Mahram, maadamu si kwa ajili ya tamaa, starehe au maslahi, ni jambo linaloruhusiwa (linajuzu). Vivyo hivyo kwa Mwanamke, ikiwa hakuna hofu ya fitina, anaweza kusikika na Wanaume wasio mahram kwake".

Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) - ABNA - Swali / Shub’ha ya Kidini: Katika ulimwengu wa leo, kutokana na ongezeko la mahusiano ya kijamii na kiuchumi, na hivyo pia kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake katika nyanja mbalimbali za kijamii, suala la mawasiliano sahihi na salama kati ya mwanamume na mwanamke limekuwa miongoni mwa masuala makuu ya kujadiliwa na watu wa dini.

Jibu:

Msingi wa kila aina ya uhusiano ni mazungumzo. Bila mazungumzo, uhusiano hauwezi kudumu na huwa hauna maana.

Kwa mtazamo wa fiqhi na maandiko ya dini, mazungumzo kati ya mwanamume na mwanamke wasio mahram siyo jambo lililokatazwa. Iwe mazungumzo hayo yanahusu masuala ya kielimu, kisiasa, au hata ya kawaida na ya kila siku, hakuna uharamu wa moja kwa moja kwa kuzungumza.

Imam Khomeini anasema:

“Kauli yenye nguvu zaidi ni hii kwamba kusikia (kusikiliza) sauti ya Mwanamke asiyekuwa Mahram, maadamu si kwa ajili ya tamaa, starehe au maslahi, ni jambo linaloruhusiwa (linajuzu). Vivyo hivyo kwa Mwanamke, ikiwa hakuna hofu ya fitina, anaweza kusikika na Wanaume wasio mahram kwake".

Baadhi ya watu wanaona kuwa ni haramu kusikia sauti ya mwanamke na kwa mwanamke kuisikia, lakini kauli hii ni dhaifu. Hata hivyo, kwa mwanamke ni haramu kuzungumza kwa namna ya kusisimua au kuchochea matamanio – yaani sauti yake isiwe nyororo, laini au ya kuvutia kiasi cha kuwashawishi wenye nyoyo dhaifu.”

Mwanazuoni mashuhuri, Sahibu al-‘Urwah al-Wuthqa, pia ametoa fatwa katika maana hiyo hiyo.

Dalili za kihistoria na riwaya nyingi zipo, zinazothibitisha kuwa wanawake walizungumza na Mtume (s.a.w.w) na Maimamu wa Ahlul Bayt (a.s). Katika matukio mengi, wanawake walikuja kwao kuuliza maswali ya kisheria, kifamilia n.k.

Kwa mfano, Bibi Fatima Zahra (s.a) na Bibi Zainab (s.a) walizungumza na Wanaume wasio Mahram katika mazingira ya wazi kabisa. Hotuba ya Bibi Zahra (s.a) katika Msikiti wa Mtume (s.a.w.w) na ile ya Bibi Zainab (s.a) huko al-Kufa na Sham, mbele ya watu wa kawaida, hata kwenye majlisi ya Yazid bin Muawia na Ibn Ziyad, ni maarufu sana.

Je, Mazungumzo Kati ya Mwanamume na Mwanamke Wasiokuwa Mahramu Yamekatazwa kwa namna yoyote ile katika Uislamu?

Ikumbukwe kuwa: Katika Uislamu, hairuhusiwi kwa Mwanaume na Mwanamke ambao sio Mahram kupeana Mikono Mubashara pasina kuwepo kizuizi chochote baina ya ngozi za mikono yao.

Riwaya zinazokataza kusalimia Wanawake:

Baadhi ya watu wanatumia riwaya zinazokataza Mwanamume kuanza kuwasalimia Wanawake kama hoja ya kuharamisha mazungumzo, lakini hoja hii ina upungufu kwa sababu:

  1. Riwaya hizo hazijagawanya kati ya wanawake mahram na wasio mahram. Ilhali ni wazi kuwa kusalimia mahram si haramu.
  2. Riwaya sahihi zinaonyesha kwamba Mtume (s.a.w) na Imam Ali (a.s) walikuwa wakianza kuwasalimia wanawake. Kwa mfano, katika hadith sahihi ya Rubi’i kutoka kwa Imam Sadiq (a.s), inasemekana:

"Mtume (s.a.w) alikuwa akiwatangulia Wanawake kwa salamu, nao walikuwa wakimjibu. Vivyo hivyo Imam Ali (a.s) alikuwa na tabia hiyo, ila alikuwa hataki sana kuwasalimia wanawake vijana, akisema: Naogopa sauti yao kunivutia, na madhara yake kuwa makubwa kuliko thawabu ya salamu hiyo."

Hadithi hii inaonyesha wazi kuwa kuwasalimia Wanawake (pasina kuwapa mikono) siyo haramu, na lau ingekuwa haramu, basi Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Maimamu Watukufu wa Kizazi cha Mtume amani iwe juu yao) wangekuwa wa kwanza kuepuka jambo hilo.


Chanzo na Marejeo:

  1. Qur'an Tukufu
  2. Nahjul Balagha
  3. Sayyid Abul Qasim al-Khu’i – Mustanad al-‘Urwah al-Wuthqa
  4. Imam Khomeini – Tahrir al-Wasilah
  5. Al-Bahrani – Al-Burhan
  6. Al-Bukhari – Sahih al-Bukhari
  7. Al-Hurr al-‘Amili – Wasail al-Shi‘ah.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha