Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) - ABNA - Samahat Sheikh Muhammad Abdu, amebainisha na kufafanua kauli Imam Ali (as) kuhusu: Kuingiza Furaha kwenye Moyo wa mtu mwenye matatizo kuwa ni bora zaidi mbele za Mwenyezi Mungu (swt). Akifafanua kauli hiyo amesema:
"Katika maneno ya Amirul-Muuminina Ali bin Abi Talib (as), anasema tena akiapa: "Naapa kwa Mwenyezi Mungu (swt), Naapa kwa yule ambaye amefunua usikivu wake ili kusikia kila aina ya sauti; Hakuna mtu yeyote atakayeingiza furaha katika moyo wa mtu mwenye matatizo, ispokuwa mtu huyo Mwenyezi Mungu (swt) ataumba kutokana na furaha ile ya mtu yule aliyoingiza katika moyo wa mtu mwingine, upole. Na mtu huyo akipatwa na matatizo, Mwenyezi Mungu (swt) atampelekea upole wake ule uondoshe matatizo yale kama vile maji yanavyotiririka kutoka katika mlima. Na utaondoa upole huo matatizo yake kama vile Farasi mgeni anavyoondolewa aingiapo katika kundi la Ngamia wengine". Haya kwa hakika ni maneno mazuri ya Amirul-Muuminina Ali bin Abi Talib (as).
Ibara zake kuhusu maneno hayo tuliyoyafafanua hapo juu katika Kiarabu kama yalivyo katika asili yake, ni haya yafuatoyo:
"فَوَالَّذِي وَسِعَ سَمْعُهُ الْأَصْوَاتَ- مَا مِنْ أَحَدٍ أَوْدَعَ قَلْباً سُرُوراً- إِلَّا وَ خَلَقَ اللَّهُ لَهُ مِنْ ذَلِكَ السُّرُورِ لُطْفاً- فَإِذَا نَزَلَتْ بِهِ نَائِبَةٌ جَرَى إِلَيْهَا كَالْمَاءِ فِي انْحِدَارِهِ- حَتَّى يَطْرُدَهَا عَنْهُ كَمَا تُطْرَدُ غَرِيبَةُ الْإِبِلِ"
Kwa hakika, haya ni maneno maridhawa ya Amirul-Muuminina Ali bin Abi Talib (as) kuhusu umuhimu wa kuleta furaha kwa wengine na jinsi Mwenyezi Mungu anavyofurahia matendo hayo na kuondoa matatizo ya mtu anayewasaidia wengine. Maneno haya yanasisitiza ushirikiano, msaada kwa wenzetu na jinsi Mwenyezi Mungu atavyolipa mema haya kwa kuondoa shida na dhiki za wale walio katika matatizo. Kwa maana: Ukitaka Mwenyezi Mungu akuondolee matatizo yako, basi jitahidi na wewe pia kuwatendea mema mengine na kuingiza furaha katika nyoyo zao.
Huna hasara yoyote hata chembe mbele ya Mwenyezi Mungu endapo utamsapoti Mwalimu kwa kumlipia mtoto wake ada ya shule na kumuepushia tatizo la mtoto wake kufukuzwa shule kwa ajili ya ada (school fees), au ukamlipia Mwalimu kodi ya nyumba, au umewalisha Mayatima na kuingiza furaha katika moyo wao, au umewasaidia wasio jiweza, n.k.
Yote hayo unayoyafanya, Mwenyezi Mungu anakuumbia upole na kuutupia ndani yako, na siku ile ambayo utapatwa na matatizo na kuwa katika hali ngumu, Mwenyezi Mungu kupitia upole ule atakushia Rehma Zake na Huruma Yake, na ataifanya ile huruma Yake na Upole Wake alioutupia ndani yako, upukutishe na kutiririsha matatizo hayo na shida hizo zilizokukumba, mithili ya maji yanavyotiririka katika mlima. Na matatizo hayo yatatondoshwa kwa mtu huyo wa kheri kama vile Ngamia mgeni anapoingia katika kundi la Ngamia wengine wenyeji na kutimuliwa".
Your Comment