16 Mei 2025 - 21:37
Source: Parstoday
Trump azitaka kampuni za US zitengeneze droni kama za Iran

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema ameziomba kampuni za Marekani kutengeneza ndege zisizo na rubani zinazofanana na droni za Iran, ambazo si ghali sana bali zina kasi ya juu na hatari.

Trump aliyasema hayo nchini Qatar jana Alhamisi kabla ya kuelekea Umoja wa Falme za Kiarabu kwa duru ya tatu na ya mwisho ya ziara yake iliyoanzia nchini Saudi Arabia mapema wiki hii. 

Trump amesema, "Niliiambia moja ya kampuni za ulinzi kwamba nahitaji ndege nyingi zisizo na rubani, na unajua, Iran inatengeneza droni nzuri, na wanazitengeneza kwa gharama ya dola 35,000 hadi 40,000." 

Ameeleza kuwa, "Kwa hiyo niliiambia kampuni hiyo, 'Nataka kuona kitu kama hicho.' Wiki mbili baadaye, walinijia na ndege isiyo na rubani ambayo iligharimu dola milioni 41! Nikasema, 'Sivyo nilivyokuwa nikizungumza. Milioni arobaini na moja?! Ninazungumza juu ya kitu ambacho kinagharimu dola 35,000 hadi dola 40,000, ili tuweze kuzirusha kwa maelfu."

Maendeleo makubwa na ya kasi ya Iran katika teknolojia ya ndege zisizo na rubani na uwezo wake wa kufanya mashambulizi ya masafa marefu katika vita vya droni kwa usahihi wa hali ya juu kumeimarisha nguvu za kijeshi za nchi hii katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Mpango wa kisasa wa ndege zisizo na rubani wa Iran umekuwa miongoni mwa mafanikio ya jeshi la taifa hili katika kutengeneza anuwai ya vifaa vya asili vya kujihami ili kufanya vikosi vya jeshi lake kujitosheleza, mkabala wa vitisho na vikwazo vya miaka mingi vya Wamarekani.

Maafisa wa Iran wameonya mara kwa mara kwamba, nchi hii haitasita kuimarisha uwezo wake wa kijeshi, ikiwa ni pamoja na uwezo wake wa makombora, ambayo ni kwa ajili ya ulinzi, wakisema uwezo wa kiulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu hautawahi kufanyiwa mazungumzo.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha