Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la AhlulBayt (a.s) -ABNA-, Amir Khan Muttaqi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Muda ya Taliban nchini Afghanistan, alisema saa chache zilizopita (Jumapili, tarehe 28 Ordibehesht) katika “Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran” kwamba kwa kipindi cha mwezi mmoja, haki ya maji ya Iran kutoka Afghanistan imekuwa ikitiririka kuelekea mikoa ya Sistan na Baluchestan nchini Iran.
Katika mazungumzo hayo, alifafanua kuwa Waziri Mkuu wa Taliban, katika ziara ya Abbas Araghchi (mjumbe wa Iran) nchini Afghanistan, alimwambia kwamba hata kama kusingekuwepo na mkataba wa maji wa Hirmand kati ya Iran na Afghanistan, wao wangaliiona kama "wajibu wa kisharia" kutowazuia Waislamu kupata maji.
Muttaqi aliendelea kusema:
"Wananchi wa Iran wasiwe na shaka kuwa hatuna nia mbaya, na tunahesabu kuwa ni wajibu wa kidini kuhakikisha maji yanawafikia Waislamu wa Iran."
Ameeleza pia kuwa sababu ya ujenzi wa mabwawa na vikwazo kwenye Mto Hirmand ni kwa lengo la kuhifadhi maji, kuzuia upotevu wake, na kuyapeleka maji hayo kwa uhitaji wa ndani pamoja na kuelekezwa Iran.
Hata hivyo, siku chache zilizopita, Gavana wa Mkoa wa Farah (mkoa unaopakana na Iran) alitangaza kwamba ujenzi wa bwawa jingine katika eneo hilo umekamilika kwa asilimia 80.
Wachambuzi wengi wanaamini kwamba ujenzi wa mabwawa ya mfululizo na Taliban upande wa magharibi mwa Afghanistan umepelekea kupungua kwa kiwango cha maji kinachoingia Iran.
Ni vyema kutaja kuwa mwaka 1351 Hijria Shamsia (1972), Iran na Afghanistan walitia saini mkataba wa maji wa Hirmand, unaotambua haki ya Iran kupokea 820 milioni za mita za ujazo za maji kila mwaka kutoka mto huo, kiwango ambacho kinaweza kubadilika kulingana na mvua na hali ya hewa ya msimu.
Your Comment