18 Mei 2025 - 20:42
Source: Parstoday
Uchunguzi: Umma wa Marekani wataka mkataba wa amani na Iran

Utafiti mpya uliofanywa nchini Marekani umeonyesha kuwa kuna uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa umma wa Marekani kwa mkataba mpya wa amani na Iran, huku kukiwa na upinzani mkubwa dhidi ya hatua yoyote ya kijeshi

Utafiti wa Critical Issues Poll uliofanywa na Chuo Kikuu cha Maryland ulibaini kuwa asilimia 69 ya Wamarekani wanataka “makubaliano ya mazungumzo yatakayopelekea mpango wa nyuklia wa Iran uendelee kwa malengo ya amani chini ya ukagauzi wa kimataifa.” Aidha, ni asilimia 14 tu waliounga mkono “hatua ya kijeshi kwa lengo la kuharibu mpango wa nyuklia wa Iran.” Asilimia 18 hawakuwa na maoni kuhusu suala hilo.

Upinzani huu mkubwa wa ndani ya Marekani dhidi ya vita na Iran unatofautiana sana na vitisho vya wazi au vya siri vinavyotolewa karibu kila siku na Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Iran. Vitisho hivyo vya Marekani vilianza baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya mwaka 1979.

Wachambuzi wanasema kwamba upinzani mkubwa wa umma wa Marekani dhidi ya vita na Iran umetokana na msimamo wa muda mrefu uliojengeka kwa miaka mingi.

Ben Zinevich kutoka chama cha Socialism and Liberation anasema kuwa baada ya kuuawa kwa Qassem Soleimani, aliyekuwa kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kulienea hofu kubwa nchini Marekani kuwa nchi hiyo ingeingia katika vita wasivyovihitaji. Luteni Jenerali Soleimani aliuawa shahidi Januari 2020 katika hujuma ya kigaidi kwa amri ya Trump.

Zinevich amesema wakati huo Wamarekani walijitokeza mitaani wakisema wazi kuwa hatutaki kabisa vita na Iran. Itakumbukwa kuwa baada ya tukio hilo Iran ilichukua hatua ya kulipiza kisasi kwa kushambulia kwa makombora kituo cha jeshi la Marekani nchini Iraq. Wamarekani walikuwa na hofu kuwa nchi yao ingeishambulia Iran kulipiza kisasi.

Mnamo mwaka 2018, Trump alijiondoa kinyume cha sheria na kwa upande mmoja katika mkataba wa JCPOA uliokuwa umejadiliwa kwa muda mrefu kuhusu mpango wa nishati ya nyuklia wa Iran. Hivi sasa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanaendelea baina ya Iran na Marekani kwa lengo la kuondoa vikwazo dhidi ya Iran.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha