28 Mei 2025 - 20:14
Source: Parstoday
Russia yajibu baada ya Trump 'kumtishia nyau' Putin eti 'anacheza na moto'

Rais wa Marekani, Donald Trump ametoa matamshi ambayo yanaonekana ya kumtishia mwenzake wa Russia, Vladimir Putin, ambapo amesema "anacheza na moto," bila kufafanua nini hasa anamaanisha.

Katika ujumbe kwenye jukwaa lake la The Social Truth jana Jumanne, Trump alidai kwamba "kama isingelikuwa mimi, mambo mengi mabaya sana yangelikuwa tayari yameikumba Russia, na ninamaanisha BAYA SANA." Rais wa Marekani aliongeza kuwa, Putin "anacheza na moto!"

Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Shirikisho la Russia, Dmitry Medvedev ametoa radimali yake kufuatia vitisho hivyo vya Trump akisema: Vita vya Tatu vya Dunia pekee ndilo "jambo BAYA SANA".

Katika siku za hivi karibuni, Trump amezidi kuikosoa Kremlin juu ya kile anachokiona kama ukosefu wa maendeleo katika mazungumzo ya amani kati ya Moscow na Kiev.

Wiki iliyopita, Trump na Putin walifanya mazungumzo kwa njia ya simu ambapo walijadili njia za suluhu ya amani kwa mzozo wa Ukraine. Hii ni katika hali ambayo, msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov alisisitiza hivi karibuni kuwa, hali ya mzozo wa Ukraine ni tata mno kiasi kwamba haiwezekani kupata mafanikio ya haraka kama vile Washington inavyotarajia.

Trump ambaye amekuwa akijitambulisha kama mpatanishi wa amani, mara kwa mara ametamka nia yake ya kukomesha “umwagaji damu” unaoendelea katika vita hivyo vya zaidi ya miaka mitatu, ambavyo sasa serikali yake inavitazama kama vita kati ya Marekani na Russia.

Mwezi uliopita, Katibu wa Baraza la Usalama la Russia Sergei Shoigu alionya kuwa, ikilazimu, Moscow itatumia haki yake ya silaha za nyuklia katika kukabiliana na mashambulio ya nchi za Magharibi.

Your Comment

You are replying to: .
captcha