Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza kuwa ipo mbioni kusaini miongozo ya kisheria itakayoweka viwango vipya vya kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Ridhiwan Kikwete, alitoa kauli hiyo Jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa jengo la biashara la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
Amesema mazungumzo tayari yamefanyika kati ya wadau, wakiwemo wamiliki wa taasisi binafsi na wasimamizi wa sera, kuhusu mapendekezo ya viwango vipya vya mshahara.
Kikao cha mwisho cha mashauriano na wadau kinatarajiwa kufanyika kabla ya serikali kusaini marekebisho hayo mapema mwezi ujao.
Waziri ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anathamini maslahi ya wafanyakazi na serikali itaendelea kuboresha sheria ili ziendane na mahitaji ya sasa.
Pia alisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wafanyakazi katika kuongeza ajira, kulinda haki zao, na kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro kupitia mazungumzo.
Serikali imedhamiria kuhakikisha wafanyakazi wa sekta binafsi wananufaika na viwango vipya vya mishahara, hatua inayotarajiwa kuboresha hali ya maisha na kulinda heshima ya kazi nchini.
Your Comment