Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Madrasa ya Kidini ya Mabanati ya Hazrat Zainab (sa), iliyopo Kigamboni Dar-es-Salaam - imeendesha kikao maalum cha tathmini ya maendeleo ya Darsa za Qur’an Tukufu na hatua za Wanafunzi katika kujifunza, kuhifadhi na kuishi mafundisho ya Kitabu Kitukufu kisichokuwa na Shaka ndani yake.
Kikao hicho maalum kilichodumu kwa dakika 45 kimehudhuriwa na walimu wote pamoja na wanafunzi wa kidini, ambapo mada kuu ilikuwa ni “Uchambuzi wa Darsa za Qur’an na Hatua Zilizopigwa.”
Kwa mujibu wa taarifa ya uongozi wa madrasa hiyo, kikao kililenga:
1_Kutathmini viwango vya usomaji na ufahamu wa Qur’an miongoni mwa wanafunzi.
2_Kupima mbinu zinazotumika na walimu katika kufundisha Tajwid, Hifdhi na Tafsir.
3_Kubaini changamoto zinazowakabili walimu na wanafunzi katika safari ya kielimu.
4_Kuweka mikakati mipya ya kuboresha ufanisi wa Darsa na kuongeza ushiriki wa wanafunzi.
Katika kikao hicho, walimu mbalimbali walitoa maoni kuhusu mbinu bora za kufundishia na kuhimiza nidhamu ya kielimu, huku wanafunzi nao wakipewa nafasi ya kueleza changamoto wanazokutana nazo.
Pia, ushauri umetolewa juu ya kuongeza masomo ya marudio na semina za Tajwid ili kuongeza kasi ya maendeleo ya wanafunzi.
Mratibu wa kikao, kwa niaba ya Madrasa ya Wasichana wa Kiislamu, aliwataka washiriki kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kufanikisha lengo kuu la kufundisha Qur’an Tukufu kwa njia sahihi na yenye matokeo ya kudumu.
Mwisho wa kikao uliambatana na dua fupi ya kuomba baraka na ufanisi zaidi katika safari ya kielimu na kiroho ya walimu na wanafunzi.
Your Comment