15 Juni 2025 - 13:17
Source: Parstoday
Dunia yalaani mashambulio ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran

Hujuma za mapema alfajiri ya jana za utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimeendelea kulaaniwa katika kila pembe ya dunia.

Nchi mbalimbali zimetoa taarifa tofauti na kusisitiza kuwa, mashambulizi ya mabomu ya usiku na mauaji ya watoto, wanawake na raia wa kawaida katika mikoa mbalimbali ya Iran ni jinai kubwa ambayo ilmerekodiwa katika historia kwa jina la utawala wa Kizayuni.

Akilaani hujuma ya kigaidi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, Cevdet Yilmaz Makamu wa Rais wa Uturuki ameitaja hatua hiyo kuwa ya kichochezi, isiyo na msingi wa kisheria na tishio jipya kwa amani na utulivu wa eneo hili.

Lin Jian, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China sambamba na kulaani unyama huo wa Israel amewaambia waandishi wa habari: "China ina wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran na matokeo yake."

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Misri pia imetoa taarifa ikiitaja hatua hiyo kuwa isiyo na uhalali na kusababisha mzozo mkubwa katika eneo hili.

Serikali ya Yemen pia imelaani vikali hujuma za wazi za utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia imesema: "Tunalaani vikali shambulio la Israel dhidi ya Iran na tunatoa wito kwa pande zote kujizuia."

Umoja wa Mataifa umetoa taarifa na kusema: Katibu Mkuu Antonio Guterres amelaani ongezeko lolote la mzozo wa kijeshi Asia Magharibi na kueleza wasiwasi wake kuhusu mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitaka pande zote mbili kujizuia.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistani imesema: "Mashambulizi ya kijeshi ya Israel dhidi ya Iran ni ukiukaji wa mamlaka na umoja wa ardhi ya Iran na yanakinzana waziwazi na Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kanuni za kimsingi za sheria za kimataifa; Iran ina haki ya kujilinda kwa mujibu wa Ibara ya 51 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa." Mataifa mengine yaliyolaani mashambulio hayo ya Israel ni Russia na Korea Kaskazini ambayo imesema kuwa iko pamoja na Iran.

Ufalme wa Saudi Arabia umezitaja hujuma hizo kama “mashambulizi ya kinyama dhidi ya taifa ndugu na la Kiislamu la Iran”, na kuitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kukomesha jinai hiyo.Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imesema: "Tunalaani kwa nguvu zote mashambulizi haya ambayo yanavunja mamlaka ya Iran na kuhatarisha usalama wake, kinyume kabisa na sheria za kimataifa.

Oman, ambayo imekuwa mpatanishi mkuu kati ya Iran na Marekani, pia imelaani mashambulizi hayo na kuulaumu moja kwa moja “utawala wa Kizayuni” kwa kuchochea mzozo huo.

Your Comment

You are replying to: .
captcha