15 Juni 2025 - 13:20
Source: Parstoday
Araghchi: Haiwezekani kuendeleza mazungumzo kati ya Iran na Marekani wakati wa unyama wa Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema kuwa kuendelea kwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, wakati ambapo utawala wa Kizayuni unaendeleza mashambulizi ya kinyama, ni jambo lisilokubalika.

Araghchi alitoa kauli hiyo Jumamosi katika mazungumzo ya simu na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, siku moja baada ya Israel kufanya mashambulizi makali dhidi ya maeneo ya kiraia na kijeshi, ikiwemo mitaa ya makaazi katika mji mkuu wa Tehran na miji mingine nchini Iran.

Mashambulizi hayo ya kinyama yamesababisha vifo vya raia wengi wasio na hatia, wakiwemo wanasayansi wa nyuklia na pia maafisa waandamizi wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika kujibu jinai hiyo Iran imeanzisha operesheni ya kijeshi  iliyopewa jina la Ahadi ya Kweli III, ambapo siku ya Ijumaa jioni ilivurumisha kwa mafanikio makombora mengi dhidi ya ngome za utawala Israel.

Katika mazungumzo hayo ya simu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani vikali vitendo vya ukiukaji wa mamlaka na ardhi ya Iran vilivyofanywa na utawala wa Kizayuni, ukiwemo uvamizi wa mitambo ya nyuklia na maeneo ya makaazi ya raia, ambavyo vimepelekea kuuliwa shahidi kwa maafisa wa kijeshi, maprofesa wa vyuo vikuu, pamoja na wanawake na watoto wa Kiirani. Ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kulaani kwa kauli kali mashambulizi hayo ya kichokozi na kuchukua hatua madhubuti dhidi ya Israel.

Aidha amesema kuwa Iran imechukua hatua za kidiplomasia za kuhamasisha jamii ya kimataifa kuhusu hatari za mienendo ya kihasama na isiyo ya kisheria ya Israel, na akautaka Umoja wa Ulaya pamoja na wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua msimamo madhubuti wa kulaani uvamizi huo na kumwajibisha mvamizi.

Araghchi, ameashiria kauli na misimamo ya Rais wa Marekani, na kusema kuwa jinai za Israel zimekuwa zikifanyika kwa baraka na uungwaji mkono wa moja kwa moja kutoka Marekani, na hivyo kuendelea kwa mazungumzo ya moja kwa moja au yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, huku ukatili wa Israel ukiendelea, hakuwezi kukubalika kwa hali yoyote ile.

Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa jibu kali dhidi ya uvamizi huo kwa lengo la kulinda mamlaka yake ya kitaifa, watu na usalama wake wa taifa, na kwamba iko tayari kutumia haki yake halali ya kujilinda na kuchukua hatua za kijeshi za kulipiza kisasi inapohitajika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya ameelezea masikitiko na hofu yake kubwa juu ya kuongezeka kwa mivutano katika eneo la Mashariki ya Kati ( Asia Magharibi). Amesema Umoja wa Ulaya uko tayari kusaidia juhudi za kidiplomasia ndani ya Baraza la Usalama na taasisi nyingine za kimataifa ili kusaidia katika kupunguza mivutano na kurejesha amani na utulivu katika eneo hili.

Your Comment

You are replying to: .
captcha