Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- kufuatia shambulio la Rahmanullah Lakanwal, mkimbizi mwenye umri wa miaka 29 kutoka Afghanistan, dhidi ya wanachama wa Walinzi wa Kitaifa wa Marekani ambalo lilisababisha kifo cha askari mmoja na kujeruhiwa kwa askari mwingine, mazingira ya kisiasa na kimediaya nchini Marekani yamejaa mivutano mikali dhidi ya wahamiaji wa Afghanistan.
Donald Trump, Rais wa Marekani, alfajiri ya Jumatatu tarehe 10 Azar*, kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye jukwaa la Truth Social, alitangaza: “Lazima tuwaondoe watu wabaya kutoka nchini mwetu, na tufanye hivyo haraka. Kile ambacho serikali ya Biden na uchaguzi wa wizi wamekitendea Marekani kamwe hakipaswi kusahauliwa.”
Wakati huohuo, Kirstjen Noem, Waziri wa Usalama wa Ndani katika serikali ya Trump, ameituhumu serikali ya Biden kuwa ndiyo inayowajibika kwa “mgogoro mbaya zaidi wa usalama wa taifa” nchini Marekani, na kusema: “Biden aliwaingiza karibu wahamiaji 100,000 wa Afghanistan bila uchunguzi, ilhali ni baada ya kuingia nchini ndio utambulisho na nia zao zilijulikana.”
Trump ametoa agizo la kufanyia mapitio upya faili zote za wahamiaji wa Afghanistan, na imetangazwa kuwa hadi mapitio hayo yatakapokamilika, ushughulikiaji wa kesi za uhamiaji utasitishwa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia imetangaza kuwa, katika mazingira ya sasa, haitatoa viza kwa wanaomiliki pasi za kusafiria za Afghanistan.
Hatua hizi zimezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa jamii ya wahamiaji wa Afghanistan waliopo Marekani, na uwezekano wa kutekelezwa sera kali zaidi katika siku zijazo umetajwa.
Your Comment