Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Beirut – Lebanon | Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Kimataifa wa Miraya, Bw. Fadi Boudieh, amesisitiza kuwa harakati za upinzani nchini Lebanon zinafuatilia kwa makini mienendo ya mjumbe wa Rais wa Lebanon pamoja na hatua za pande zote husika, ili kuzuia jaribio lolote la kuingia katika mtego wa uhalalishaji wa mahusiano (normalization) na utawala wa Kizayuni.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel imedai kuwa Benjamin Netanyahu ameagiza kutumwa kwa ujumbe maalumu wa Israel kukutana na maafisa wa serikali ya Lebanon. Taarifa hiyo ilitangazwa kupitia mtandao wa kijamii wa X, ikidai kuwa mkutano huo ni jaribio la kwanza la kuweka msingi wa mahusiano ya kiuchumi kati ya pande hizo mbili.
Tangazo hilo lilitolewa baada ya Rais wa Lebanon kumteua raia (asiye wa kivita) kuwa mkuu wa ujumbe wa Lebanon katika kamati ya watu watano inayosimamia utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Wakati huo huo, taarifa kuhusu mazungumzo ya kiuchumi kati ya Lebanon na Israel zilichochea maandamano makubwa kusini mwa mji wa Beirut, ambapo waandamanaji walipinga vikali aina yoyote ya maridhiano na serikali yao na utawala wa Kizayuni. Waandamanaji walielezea hatua hizo kama njama ya kuelekea kwenye uhalalishaji wa mahusiano na Israel, wakitaka mazungumzo yote yasiyo ya wazi yasitishwe mara moja.
Israel Inajaribu Kudanganya Dunia – Boudieh
Katika mazungumzo yake na ABNA, Fadi Boudieh alisema kuwa bila shaka Israel inajaribu kuwapotosha baadhi ya Walebanoni, Waisraeli na hata baadhi ya nchi za Kiarabu, kwa kuwashawishi kuwa imefanikiwa kulazimisha hali mpya ya kiuchumi kwa Lebanon kwa kutumia nguvu, na kwamba chaguo la upinzani (Muqawama) limekwisha.
Aliongeza kuwa Israel inajaribu kulifanya jamii ya kimataifa, wananchi wa Lebanon na Waisraeli waamini kuwa kuwepo kwa raia katika ujumbe wa mazungumzo ni ishara ya kuanzishwa kwa mahusiano ya kiuchumi. Kwa mujibu wa Boudieh, Israel imekuwa ikijaribu kuanzisha uhusiano wa kibiashara kupitia baadhi ya wawakilishi wa kimataifa ili kupenya ndani ya Lebanon.
Amesisitiza kuwa Israel ni adui wa Lebanon, na hakuna uwezekano wa kuwepo kwa mkataba wa amani, uhalalishaji wa mahusiano au aina yoyote ya uhusiano na adui huyu. Ameitaja Israel kuwa dola bandia, ya kikoloni na ya upanuzi, ambayo haianzishi mahusiano kwa faida ya wengine bali kwa maslahi yake ya kiupanuzi.
Lengo Kuu ni Kudhibiti Uchumi wa Kanda na Rasilimali za Bahari ya Mediterania
Boudieh amesema Israel kwa muda mrefu imekuwa ikilenga kudhibiti uchumi wa eneo kupitia njia za maji na biashara ya baharini. Kwa mtazamo wake, Israel ina tamaa kubwa ya rasilimali za mafuta na gesi katika Bahari ya Mediterania na inalenga kuzidhibiti kikamilifu kupitia Cyprus, Ugiriki, Syria na Lebanon.
Amesisitiza kuwa uhalalishaji wa mahusiano na Israel hauwezekani kwa namna yoyote, kwani ni dola yenye tabia ya kumeza nchi za wengine na kutawala maeneo yote kisiasa, kiuchumi na kijiografia. Ameongeza kuwa Israel haijawahi kuheshimu mikataba yoyote, na ushahidi mkubwa ni uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza.
Hakuna Kikao cha Kiuchumi – Majukumu ni ya Kisiasa na Kiusalama
Boudieh amebainisha kuwa Israel inatumia neno “mkutano wa kiuchumi” kwa propaganda, ilhali ujumbe wa Lebanon una majukumu manne tu:
- Kushughulikia masuala yaliyosalia kati ya Lebanon na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu
- Kuhakikisha kuachiliwa kwa wafungwa
- Kujadili kusitishwa kwa mapigano
- Kuendeleza mchakato wa uwekaji wa mipaka ya baharini
Ameeleza wazi kuwa hakuna maudhui yoyote ya kiuchumi katika vikao hivyo.
Upinzani Ndio Kikwazo Kikuu cha Uhalalishaji
Mchambuzi huyo amesisitiza kuwa kile kinachozuia Lebanon kuingia kwenye uhalalishaji wa mahusiano na Israel ni uwepo wa harakati ya upinzani. Amesema kuwa wito wa kuondolewa silaha za upinzani ni hatua ya wazi kuelekea uhalalishaji.
Ameongeza kuwa upinzani umejitolea kwa kutoa makumi ya maelfu ya mashahidi kwa ajili ya kuikomboa Lebanon na kulinda utambulisho wake wa Kiarabu ambao hauwezi kamwe kuunganishwa na Israel.
Upinzani Bado Uko Tayari kwa Mapambano
Boudieh amesema kuwa upinzani umeipa serikali fursa ya kidiplomasia ya kuiondoa Israel ndani ya mwaka mmoja, lakini serikali imeshindwa. Katika kipindi hicho, upinzani umeendelea kujijenga upya kijeshi na kusisitiza kuwa haitatoa silaha zake hadi Israel iondoke kabisa na kuwepo dhamana ya kweli ya kutoendelea kwa uchokozi.
Amehitimisha kwa kusema: “Upinzani hautokubali mazungumzo yoyote yanayolenga uhalalishaji wa mahusiano na Israel, na endapo vita vitatulazimishwa, tuko tayari kukabiliana navyo.”
Your Comment