Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Katika mazingira ya mjadala unaozidi kushika kasi duniani kuhusu kuchanganywa kwa Uyahudi kama dini na Uzayuni kama harakati ya kisiasa, na huku serikali ya uvamizi ya Israel ikiendelea kudai na kujitambulisha kama “dola inayowakilisha Wayahudi”, wakati vita vya mauaji ya kimbari na uvamizi wa ardhi za Palestina vinaendelea, sauti ya rabi wa Kiyahudi wa kidini anayepinga simulizi hili imejitokeza wazi.
Katika mahojiano maalumu na tovuti ya Arabi21, rabi wa Kiyahudi anayehusishwa na shirika la Neturei Karta linalopinga Uzayuni, alieleza tofauti ya msingi kati ya Uyahudi na Uzayuni, akisisitiza kuwa uhalifu unaotekelezwa dhidi ya Wapalestina hauwakilishi dini ya Kiyahudi, bali unaathiri vibaya Wayahudi duniani kote.
Rabi David Feldman aliuelekeza ujumbe wa moja kwa moja kwa vijana wa Kiyahudi wanaoishi chini ya uvamizi wa Israel, akiwataka wakimbie katika dola hilo, akionya kuwa kuendelea kwa vita vya mauaji ya kimbari hakuwahatarishi Wapalestina na Waislamu pekee, bali pia kunaongeza hatari ya chuki na vurugu dhidi ya Wayahudi katika nchi mbalimbali duniani. Pia alieleza msimamo wake kuhusu mjadala wa sasa wa suluhisho la mataifa mawili. Ifuatayo ni mazungumzo kamili:
Swali: Tafadhali jitambulishe na utuambie kuhusu shirika unalotoka
Jibu: Jina langu ni Rabi David Feldman, nami ni mwanachama wa shirika la kimataifa la Neturei Karta. Sisi ni shirika la kidini la Kiyahudi duniani kote, tunawakilisha sauti ya makundi makubwa ya Wayahudi wanaopinga falsafa ya Uzayuni, dola la Israel, na uhalifu wote unaofanywa dhidi ya Palestina.
Swali: Unaonaje kinachoendelea Palestina?
Jibu: Kinachoendelea Palestina si uhalifu tu kwa mujibu wa sheria za kimataifa, wala si ukiukwaji wa viwango vyote vya haki za binadamu pekee, bali pia ni uhalifu kwa mujibu wa dini ya Kiyahudi. Kuua, kuiba, na kuwatesa watu wote kwa ujumla ni makosa kwa mujibu wa mafundisho ya Kiyahudi, hasa yanapofanyika Palestina. Watu hao (Wapalestina) walituheshimu na tulikuwa chini ya ulinzi wao kwa muda mrefu, hadi miaka ya 1920 pale Uzayuni ulipoingia katika ardhi takatifu. Kinachotokea ni kosa, nasi tunajaribu kuwasaidia watu kuvuka propaganda za Kizayuni na kuelewa kuwa kupinga uhalifu huu haimaanishi kuwa wapinzani hao ni maadui wa Uyahudi au wanachukia Wayahudi.
Swali: Je, Israel inawakilisha Wayahudi wote duniani?
Jibu: Dola la Israel haliwakilishi Wayahudi wote, na kwa hakika haliwakilishi dini ya Kiyahudi. Makundi makubwa ya Wayahudi duniani yanapinga uhalifu huu wote, na dini ya Kiyahudi yenyewe inapinga uhalifu huo. Watu wenye dhamira hai, waadilifu na waaminifu, wanapaswa kuinua sauti zao tunaposhuhudia mbele ya macho yetu zaidi ya miaka miwili ya mauaji ya kimbari ambayo bado hayajasimama.
Swali: Je, Wayahudi wanaathirika vipi na vitendo vya Israel huko Palestina?
Jibu: Kwa masikitiko makubwa, watu wanauawa, watoto wananyimwa chakula hadi kufa, na kwa bahati mbaya hali hii bado inaendelea. Tunapaswa kufanya kila tuwezalo kubadili hali hii, kukomesha uvamizi, kuleta haki kwa watu wa Palestina, na usalama kwa Wayahudi, kwa sababu Wayahudi wanakumbana na matokeo, chuki na hatari kutokana na vitendo vyote vinavyofanywa kwa jina lao. Tunalaani harakati ya Uzayuni na dola la Israel, si tu kwa idadi kubwa ya uhalifu dhidi ya Palestina, bali pia kwa kuwaweka Wayahudi katika hatari kwa kusisitiza kufanya uhalifu huo kwa jina la jamii yote ya Kiyahudi.
Swali: Kuna tofauti gani kati ya Uzayuni kama itikadi na Uyahudi kama dini?
Jibu: Ni muhimu sana kuelewa tofauti kubwa kati ya Uyahudi na Uzayuni. Uyahudi ni dini, dini tu, inayojengwa juu ya kumuamini Mwenyezi Mungu na kutekeleza amri Zake. Hauna siasa, hauna utaifa, na kwa hakika hauna uhalifu. Uzayuni, kwa upande mwingine, ni harakati ya kisiasa iliyoanzishwa na watu wasiokuwa watii wa sheria za Uyahudi, na wanautumia vibaya dini wanayoikataa ili kuhalalisha uhalifu ambao ni haramu ndani ya dini hiyo hiyo.
Swali: Mnaupinga vipi Uzayuni unaochafua taswira ya Uyahudi?
Jibu: Uzayuni ni hatari kwa ubinadamu na ni kudhalilisha jina la Mwenyezi Mungu. Njia yetu ya kupambana nao ni kupitia elimu na uhamasishaji. Watu wengi wanakosa taarifa za msingi, na vyombo vikuu vya habari havitoi ukweli wa kutosha. Sisi tunafundisha, tunaeneza uelewa, na tunaeleza mafundisho ya Uyahudi kuhusu hali hii, ili kuwasaidia watu kuvuka propaganda na kuelewa kuwa kusimama upande wa haki na uadilifu si chuki dhidi ya Wayahudi.
Swali: Je, hili linahusiana na suala la kulazimishwa kwa Wayahudi wa dini kujiunga na jeshi la Israel?
Jibu: Vijana wa kidini wanaokataa kujiunga na jeshi hawaiamini Israel. Wanapinga kushiriki katika uhalifu huu. Kwa masikitiko, vijana hao wanahesabiwa kama wahalifu wanapofikisha umri wa miaka 17 kwa sababu tu hawajiungi na jeshi. Nina rafiki aliyekimbia Israel, lakini watoto wake wawili hawawezi kuondoka kwa sababu watakamatwa mara tu wakifika uwanja wa ndege.
Swali: Unaonaje mapambano yanayoendelea Gaza?
Jibu: Hali ni mbaya sana. Hili halikuanza leo, wala jana, wala miaka miwili iliyopita, bali lilianza pamoja na mwanzo wa Uzayuni takribani miaka 100 iliyopita. Bila kushughulikia mzizi wa tatizo ambao ni uvamizi, hakuna mwisho unaoonekana.
Swali: Ujumbe wako kwa vijana wa Israel ni upi?
Jibu: Ni wakati wa kuamka na kutambua kuwa ahadi za Uzayuni kuhusu usalama na makazi ya Wayahudi zilikuwa za uongo tangu mwanzo. Mfumo huu ni hatari kwa kila mtu, wakiwemo Wayahudi wenyewe. Nawahimiza Wayahudi wote waondoke, kwa sababu maisha yao, hali yao ya kiroho, na Uyahudi wao viko hatarini.
Swali: Je, mnakubali suluhisho la mataifa mawili?
Jibu: Hapana. Sehemu inayorejeshwa kwa Wapalestina ninaikubali, lakini sehemu itakayobaki mikononi mwa mashirika ya Kizayuni siikubali. Tunapaswa kumaliza uvamizi wa Kizayuni kabisa, kurejesha haki zote, kuruhusu wakimbizi warudi, na kuwaacha Wapalestina waamue mustakabali wa nchi yao.
Swali: Unaionaje hatima ya ardhi hiyo?
Jibu: Historia inaonyesha kuwa utawala wa Kiislamu uliwalinda Wayahudi na ulikuwa wa haki. Serikali ya Kiislamu, hata ya kidini, itakuwa bora zaidi kuliko hali ya sasa, na itaheshimu Uyahudi zaidi.
Swali: Unasemaje kuhusu juhudi za Waarabu na Marekani kuunga mkono Israel?
Jibu: Inasikitisha kuona uungaji mkono wa upofu kwa Israel. Tunawahimiza wanasiasa kuvuka propaganda na kusimama upande wa ubinadamu na haki.
Your Comment