21 Desemba 2025 - 22:45
Kuanzia Panama 1989 hadi Venezuela 2025; Kurudiwa kwa Sera ya Uingiliaji wa Marekani katika Amerika ya Kusini

Uingiliaji huu, ambao mara nyingi umelaaniwa na jumuiya ya kimataifa, umezaa matokeo ya kudumu kama vile ukosefu wa utulivu, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kudhoofishwa kwa uhuru wa mataifa - hali inayosisitiza tena umuhimu wa kuheshimu sheria za kimataifa na kupinga sera za upande mmoja zinazoathiri amani ya kikanda.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Kuongezeka kwa mashinikizo ya Marekani dhidi ya Venezuela - ikiwemo kuzingirwa kwa njia ya bahari, kunaswa kwa meli za mafuta na kutoa tuhuma za biashara ya dawa za kulevya - kunakumbusha kwa kiasi kikubwa uvamizi wa kijeshi wa nchi hiyo dhidi ya Panama mwaka 1989. Huu ni mfano unaojirudia wa sera ya uingiliaji wa Marekani, ambayo katika miongo kadhaa iliyopita imesababisha vifo vya mamia ya maelfu ya raia wasio na hatia na kuweka mbele maslahi ya kimkakati ya Washington kuliko uhuru wa mataifa.


Kwa mujibu wa uchambuzi wa matukio ya hivi karibuni katika Amerika ya Kusini, inaonekana wazi kuwa sera za Marekani za kuingilia masuala ya ndani ya serikali huru za eneo hili zina historia ndefu, huku mifano ya zamani ikiendelea kujirudia katika sera ya kigeni ya Washington hadi leo.


Uvamizi wa Panama; hatua muhimu ya uingiliaji wa kijeshi wa Marekani Mnamo Desemba 1989, Rais wa wakati huo wa Marekani, George Bush Mzee, alitoa amri ya kutekelezwa kwa operesheni iliyopewa jina la “Just Cause”. Katika operesheni hiyo, takribani wanajeshi 30,000 wa Marekani waliingia Panama kwa lengo la kumuondoa Jenerali Manuel Noriega, aliyekuwa mtawala wa nchi hiyo. Noriega hapo awali alikuwa mshirika wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), lakini baadaye alilengwa kwa madai ya biashara ya dawa za kulevya.
Takwimu rasmi za Marekani zilitangaza idadi ya raia wa Panama waliouawa kuwa 202, lakini vyanzo huru - ikiwemo mashirika ya haki za binadamu na taasisi za ndani - vimekadiria idadi ya waliopoteza maisha kuwa kati ya 300 hadi maelfu kadhaa. Maeneo kama El Chorrillo yaliharibiwa karibu kabisa kutokana na mabomu na moto mkubwa.


Hukumu ya kimataifa na historia ndefu ya mapinduzi
Umoja wa Mataifa ulitangaza uvamizi huo kuwa ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, huku Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likiupinga kwa kura 75. Tukio hili linaangukia ndani ya historia ndefu ya uingiliaji wa Marekani katika Amerika ya Kusini; kuanzia “Vita vya Ndizi” hadi mapinduzi yaliyoungwa mkono na Washington nchini Guatemala (1954), Chile (1973) na Nicaragua—yote yakilenga kudhibiti serikali huru na rasilimali za kimkakati.

Kuanzia Panama 1989 hadi Venezuela 2025; Kurudiwa kwa Sera ya Uingiliaji wa Marekani katika Amerika ya Kusini

Wanajeshi wa Marekani pindi walipo ivamia Panama mwaka 1989


Venezuela 2025; kurudiwa kwa mtindo uleule
Mwaka 2025, serikali ya Donald Trump imefuata mkondo kama huo dhidi ya Venezuela. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuzingirwa kikamilifu kwa njia ya bahari, kunaswa kwa meli mbili za mafuta ya Venezuela katika maji ya kimataifa, na kutoa tuhuma dhidi ya Rais Nicolás Maduro kwamba anaongoza kile kinachoitwa “genge la narco-terrorism”—tuhuma ambazo hadi sasa hazijaungwa mkono na ushahidi wa kuthibitisha.


Mashinikizo hayo yamesababisha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa mauzo ya nje ya mafuta ya Venezuela, huku ripoti zikieleza kuwepo kwa hitilafu katika mifumo ya GPS katika eneo la Karibiani, jambo lililozua hofu kuhusu usalama wa anga na usafiri wa baharini.


Mfumo usiobadilika katika sera ya kigeni ya Marekani
Sera hii haijabaki Amerika ya Kusini pekee, bali imeonekana pia katika migogoro mingine mikubwa iliyoongozwa na Marekani. Vita vya Vietnam (1955–1975) vilisababisha vifo vya takribani raia milioni mbili wa Vietnam. Aidha, uvamizi wa Iraq mwaka 2003, kwa mujibu wa vyanzo kama Iraq Body Count, ulipelekea vifo vya zaidi ya raia 200,000 kutokana na ghasia za moja kwa moja.


Maslahi ya kimkakati dhidi ya uhuru wa mataifa
Ulinganisho wa matukio haya unaonesha uthabiti wa sera ya kigeni ya Marekani: kutumia visingizio kama vita dhidi ya dawa za kulevya au kueneza demokrasia, ilhali lengo kuu ni kufikia rasilimali za kimkakati na kubadilisha tawala huru. Mfereji wa Panama katika miongo iliyopita na akiba kubwa ya mafuta ya Venezuela leo ni mifano hai ya maslahi hayo.


Uingiliaji huu, ambao mara nyingi umelaaniwa na jumuiya ya kimataifa, umezaa matokeo ya kudumu kama vile ukosefu wa utulivu, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kudhoofishwa kwa uhuru wa mataifa - hali inayosisitiza tena umuhimu wa kuheshimu sheria za kimataifa na kupinga sera za upande mmoja zinazoathiri amani ya kikanda.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha