Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa salamu za Sikukuu ya Krismasi kwa Wakristo wote nchini pamoja na Watanzania kwa ujumla.
Rais Samia amesema: “Ninawatakia kheri ya Sikukuu ya Krismasi Wakristo na Watanzania wote. Mnaposafiri na kujumuika na ndugu, jamaa na marafiki katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, tusherehekee sikukuu hii kwa furaha, amani na upendo.”
Ameongeza kuwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo iwe ni fursa ya kutafakari na kuimarisha maadili mema katika jamii, akisema:
“Kuzaliwa kwa Yesu Kristo kutukumbushe upendo kwa Mwenyezi Mungu, upendo kwa kila mmoja wetu, pamoja na wajibu wa kujitoa kuwasaidia wenye uhitaji, kuishi kwa uvumilivu na unyenyekevu.”
Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kuendelea kulilinda Taifa la Tanzania kwa pamoja ili lidumu katika misingi ya:
1_Amani na utulivu
2_Haki na ukweli.
3_Maendeleo na ustawi wa wananchi wote - kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Amehitimisha kwa dua akisema: “Mwenyezi Mungu awabariki nyote.”
Your Comment