25 Desemba 2025 - 22:25
Mahmoud Al-Hashimi: Hoja 23 Muhimu Kuhusu Mradi wa Kiamerika wa “Kuhodhi Silaha Mikononi mwa Serikali”

Mchambuzi wa masuala ya Iraq, katika kumbukumbu maalumu kwa Shirika la Habari la ABNA, aliandika: “‘Kuhodhi silaha mikononi mwa serikali’ kunahitaji kuwepo kwa serikali halisi; lakini ni vipi raia wa Iraq anaweza kuamini kuwepo kwa serikali kama hiyo, ilhali wabunge wengi wa Bunge la Taifa, chini ya shinikizo la Marekani, waliondoka kwenye ukumbi wa Bunge ili kuzuia upigaji kura kuhusu sheria ya Hashd al-Shaabi?”

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Katika siku za hivi karibuni, Mfumo wa Uratibu wa Iraq unaendelea na mashauriano ya kumteua Waziri Mkuu na pia kujadili suala la kuhodhi silaha mikononi mwa serikali. Habari kinzani kuhusu kauli za wanasiasa na makundi ya Muqawama zimekuwa zikizunguka katika vyombo vya habari.


“Faiq Zaidan”, Rais wa Baraza Kuu la Mahakama la Iraq, alidai kuwa viongozi wa makundi ya Muqawama (bila kuyataja kwa majina) wametangaza kukubaliana kushirikiana katika suala la kuhodhi silaha mikononi mwa serikali.


Hali hii ni wakati ambapo Kata’ib Hezbollah ilitoa tamko la kupinga kuvuliwa silaha na kusisitiza kuwa kupatikana kwa mamlaka kamili na usalama wa kweli wa Iraq ni sharti la msingi kabla ya hatua kama hiyo kuchukuliwa.


Katika muktadha huo, “Mahmoud Al-Hashimi”, mchambuzi wa masuala ya Iraq, aliandika yafuatayo:

1_ Vyama na miungano ya kisiasa ya Iraq inayoshiriki katika mchakato wa kisiasa haina mfumo thabiti, wa kitaalamu na wenye malengo ya wazi katika vyombo vya habari; kiasi kwamba wanapotaka kusukuma mbele wazo au uamuzi fulani, hushindwa kuusindikiza kwa uwasilishaji mzuri wa habari unaotegemea hoja na mitazamo imara. Upungufu huu wa vyombo vya habari huwapa wapinzani wao fursa ya kuunda simulizi na “uonyeshaji” wa suala husika kulingana na mielekeo na maslahi yao wenyewe.


2_Vyama na mikondo ya kisiasa ya Iraq pia vinakosa taasisi madhubuti za fikra, utafiti na ushauri; hivyo basi, maamuzi na mielekeo yao mara nyingi huchukuliwa bila utafiti wa kina na uchambuzi wa kutosha. Hali hii huzalisha misimamo inayosababisha si tu kuyumba kwa utendaji wao, bali pia kuweka malengo wanayotaka kuyafikia katika hali ya utata na mkanganyiko.


3_Tangazo la uamuzi wa “kuhodhi silaha mikononi mwa serikali” lilitolewa katika mazingira yasiyo na manufaa kwa mhimili wa Muqawama; kwa kuwa kipindi hiki kiliambatana na ongezeko la mashinikizo kutoka Marekani na Israel ya kusukuma mbele mkabala huo dhidi ya mihimili yote ya Muqawama. Matokeo yake ni kwamba uamuzi huo uliuweka Muqawama chini ya shinikizo la ziada, na zaidi ya hapo, maadui wa ndani na nje waliutumia kama kisingizio cha kuendeleza na kuongeza mashinikizo yao; kwa kuwa sasa wamepata hoja na uhalalisho wa kufuatilia matakwa yao.


4_Kutolewa kwa matamko kutoka kwa makundi mengine ya kupinga uamuzi huu kumeonesha wazi kuwa makundi ya Muqawama hayapo katika msimamo mmoja, na suala la “kuhodhi silaha” kwa hakika limefichua kukosekana kwa angalau kiwango cha chini cha uratibu miongoni mwao.


5_Mgawanyiko huu katika mtazamo wa vikosi vya Muqawama, kwa kawaida, utaendelea hadi katika maamuzi ya kisiasa pia; hususan katika hali ambayo hapo awali, Wa-Iraq wengi walifurahishwa na kuundwa kwa Bunge jipya lenye takribani viti 90 vinavyohusishwa na mkondo wa Muqawama.


6_Kuliibuliwa kwa suala la “kuhodhi silaha” kwa namna hii kumezua mjadala mpana na mvutano mkubwa katika miduara ya kisiasa, miongoni mwa wasomi wa fikra na utamaduni, na pia katika jamii na fikra za umma wa Iraq.


7_Suala hili pia limegeuka kuwa changamoto ya ndani ndani ya miungano ya kisiasa na vikosi vya Muqawama; na hilo limetokea katika wakati ambapo jamii ya Iraq ilikuwa inasubiri kutangazwa rasmi kwa kuundwa kwa serikali mpya.


8_Kuingilia kwa Rais wa Baraza Kuu la Mahakama, Bw. Faiq Zaidan, katika suala la “kuhodhi silaha” kumezua mtazamo kuwa kana kwamba wahusika waliotangaza uamuzi huu waliitegemea zaidi ushauri binafsi wa mkuu wa mhimili wa mahakama, badala ya uamuzi wa kimkakati uliopimwa, kujadiliwa na kukubaliwa kwa pamoja na pande zote; yaani haukuwa matokeo ya uamuzi wa pamoja uliofikiwa baada ya utafiti na maridhiano ya wahusika wote.


9_ Raia wa Iraq hulielewa “Muqawama” kama mchanganyiko wa silaha na siasa kwa pamoja, na kwa msingi huo ameshiriki katika uchaguzi; kwa kuwa kwa mtazamo wake, silaha ya Muqawama ina jukumu la kulinda nchi na mamlaka ya kitaifa.


10_Uamuzi huu ulitolewa katika kipindi ambacho Marekani ilichapisha hati yake ya usalama wa taifa katika ripoti ya kurasa 33, bila hata kulitaja jina la Iraq. Katika hati hiyo ilisisitizwa kuwa Mashariki ya Kati siyo tena miongoni mwa vipaumbele vikuu vya Marekani, kiasi kwamba hata mafuta ya eneo hilo hayachukuliwi tena kuwa ya lazima. Aidha, Marekani ilitangaza kuwa haina jukumu la kubadilisha mifumo ya kisiasa ya eneo hili, bali hushughulika nayo kama “uhalisia uliopo”.


11_Uamuzi huu pia ulifuatia tamko la Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani lililosisitiza kuwa wizara hiyo na serikali ya Marekani hazihusiki na kauli za mwakilishi wa Rais wa Marekani (Safaya), na kwamba yeye si chochote zaidi ya mtu aliyetoa huduma fulani kwa Rais wa Marekani wakati wa uchaguzi, na Rais pia akaona inapendeza kumshukuru kwa namna fulani.


12_Ilipaswa suala la “kuhodhi silaha” kwanza liwasilishwe kama wazo la ndani kutoka kwa mojawapo ya makundi ya Muqawama, na katika hatua ya awali lijadiliwe miongoni mwa makundi hayo yenyewe; kisha liwasilishwe kwa vikosi vya Mfumo wa Uratibu, ili baada ya mjadala, utafiti na uchambuzi wa kina, iwezekane kufikia matokeo chanya na yanayokubaliwa kwa pamoja.


13_Msimamo wa vyombo vya habari vinavyounga mkono suala la “kuhodhi silaha” haukutofautiana na ule wa vyombo vya habari vinavyolipinga; vyote vililishughulikia kana kwamba ni “burudani ya vyombo vya habari”. Katika muktadha huo, waliwakutanisha sura zinazopingana na zisizopatana, na kuunda taswira ya “mapigano ya majogoo”, bila kupatikana matokeo yoyote yenye uzito au manufaa kwa msingi wa suala lenyewe.


14_Haiwezi kukanushwa kuwa idadi kubwa ya watu wanaamini kuwa tangazo la mradi wa “kuhodhi silaha” lilitolewa chini ya shinikizo la moja kwa moja la Marekani.


15_Masharti yaliyotolewa na mwakilishi wa Rais wa Marekani (Safaya) baada ya kutangazwa kwa “kuhodhi silaha” yanafikia hata kuvuliwa silaha binafsi kwa raia. Hii ina maana kwamba yeyote anayefikiri hatua kama hiyo inaweza kupunguza mashinikizo katika mchakato wa kisiasa wa nchi anakosea; kwa kuwa Wamarekani hawatosheki, daima huongeza masharti na kutamani madai zaidi.


16_Wanasiasa wote waliotangaza mradi wa “kuhodhi silaha” walisisitiza kuwa huu ni “uamuzi wa kisiasa wa Iraq”; hata hivyo, swali la msingi ni: ikiwa ni hivyo, kwa nini suala hili nyeti halikujadiliwa miongoni mwao kabla ya kutangazwa hadharani, kiasi cha kuwashangaza wengi?

17_Haiwezi kukanushwa kuwa kutangazwa tu kwa suala la “kuhodhi silaha” kutaathiri moja kwa moja mwelekeo wa jumla wa Hashd al-Shaabi.


18_Taasisi ambayo kwa msisitizo mkubwa imekuwa ikiitaka tabaka la kisiasa la Iraq na serikali zake zivue silaha za Muqawama na kulivunja Hashd al-Shaabi ni Marekani; ilhali nchi hiyo hiyo ina vikundi 35 vya wanamgambo wasio rasmi, na ina kiwango kikubwa zaidi cha silaha binafsi duniani, kiasi kwamba silaha binafsi zilizo mikononi mwa raia wa Marekani ni sawa na nusu ya silaha zote binafsi zilizopo duniani. Pamoja na hayo, serikali za Marekani mfululizo zimeshindwa kudhibiti hatari hii; hatari ambayo kila mwaka husababisha vifo vya maelfu ya watu wasio na hatia.


19_“Kuhodhi silaha mikononi mwa serikali” kunahitaji kuwepo kwa serikali halisi; lakini ni vipi raia wa Iraq anaweza kuamini kuwepo kwa serikali kama hiyo, ilhali wabunge wengi wa Bunge la Taifa, chini ya shinikizo la Marekani, waliondoka kwenye kikao cha Bunge ili kuzuia upigaji kura kuhusu sheria ya Hashd al-Shaabi?

20_Serikali ya Iraq mwaka 2014 ilishindwa mbele ya uvamizi wa Daesh katika mikoa ya magharibi, ikaacha silaha zake hadi wanachama wa Daesh wakazitumia hizo silaha kufanya gwaride katika mitaa ya Ninawa. Ni Muqawama na silaha za Muqawama ndizo zilizofufua tena serikali na kurejesha uhai wa mamlaka yake.


21_Muqawama ni haki halali; mradi tu majeshi ya uvamizi yapo katika ardhi ya Iraq, na hadi pale ambapo majeshi ya kigeni ya Uturuki yanaendelea kukalia sehemu za mkoa wa Kurdistan, kufanya mauaji, kusababisha uhamishaji wa watu, uchomaji moto na uporaji wa rasilimali.


22_Suala la Palestina bado liko katika kiini cha fikra za jamii ya Iraq, na mapambano ya Tufani ya Al-Aqsa bado yanaendelea na yanahitaji msaada na uungaji mkono. Sisi si miongoni mwa wale wanaotazama hali hii kwa kusema: “tumeiepusha nchi yetu na vita”; kwa kuwa lugha kama hiyo ni ishara ya kushindwa na kukana thamani za kidini na kimaadili.


23_Tunaamini kuwa misimamo iliyotangazwa na vikosi vya Muqawama yote imechukuliwa kwa nia njema. Vikosi vyote vina historia ya jihadi na kujitolea kwa kiwango kikubwa, na kwa mtazamo wetu, hakuna hata kimoja kinacholenga kuvuliwa silaha au kupunguzwa kwa silaha zake kwa namna ya kweli; kwa kuwa njia iliyo mbele bado ni ndefu.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha