Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ataomba apatiwe muda zaidi kuunda serikali mpya-ofisi ya rais imesema hii leo.Baada ya kushinda kwa mshangao mkubwa uchaguzi,Netanyahu aliombwa Marchi 25 iliyopita na rais Reuven Rivlin aunde serikali mpya katika kipindi cha wiki 4 zilizofuatia.Wakati tarehe hiyo inakurubia,kiongozi huyo wa Israel anapanga kukutana na rais Rivlin kesho na kumuomba rasmi ampatiwe wiki mbili zaidi.Kwa mujibu wa sheria msingi,rais ana madaraka ya kufanya hivyo.Pindi Netanyahu akishindwa baadae kuunda serikali ya muungano,rais Rivlin anaweza kumteuwa kiongozi wa chama chengine kuunda serikali mnamo muda wa siku 28.Na hilo likishindikana,kiongozi wa tatu atakuwa na wiki mbili tu kutekeleza jukumu hilo-akishindwa rais ataitisha uchaguzi mkuu.Tangu alipochaguliwa Benjamin Netanyahu alikuwa akitaraji kuunda serikali ya muungano kati ya chama chake cha mrengo wa kulia, Likud,kilichojikingia viti 30, chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Nyumba ya wayahudi,viti vinane,chama kinachopalilia chuki dhidi ya waarabu Israel Beitenu,viti sita , kile cha nadharia kali za Orthodox Shas na kile cha Muungano wa Taurat,viti 6 na cha mrengo wa kati kulia Kulanu viti 10.