25 Januari 2017 - 20:26
Majeshi ya Iraq yakomboa Eneo la mashariki la Mosul kutoka kwa magaidi wa Daesh

Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi ametangaza rasmi kukombolewa upande wa mashariki wa mji wa Mosul ambao hapo awali ulikuwa ukidhibitiwa na wanapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh linalojiita Dola la Kiisilamu ambalo linauhusiano wa karibu na Saudia arabia.

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Waziri Mkuu wa Iraq  Haider al-Abadi  ametangaza rasmi kukombolewa upande wa mashariki wa  mji wa Mosul ambao hapo awali ulikuwa ukidhibitiwa na wanapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh linalojiita Dola la Kiisilamu ambalo linauhusiano wa karibu na Saudia arabia.

Vikosi vya Iraq vimefanikiwa kuwaondosha wanamgambo wa kundi hilo la kigaidi kutoka katika ngome yao ya mwisho katika eneo la mashariki la mji huo kwa msaada mkubwa wa washauri wa mambo ya kijeshi kutoka Iran, wakati mashirika ya misaada yakikadiria kiasi ya watu 750,000 bado wako katika eneo la magharibi la mji huo ambalo bado linadhibitiwa na kundi la kigaidi la Daesh.

Katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari Waziri Mkuu Haider al- Abadi alivisifu vikosi vyote vya usalama vilivyofanikisha operesheni hiyo pamoja na umma kwa kuunga mkono operesheni hiyo.

Mji wa Mosul ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Iraq na ngome kuu ya mwisho ya kundi la kigaidi la Daesh nchini Iraq uliangukia chini ya mikono ya kundi hilo wakati wa majira ya kiangazi mnamo mwaka 2014 wakati kundi hilo lilipoyashikilia  maeneo makubwa kaskazini na magharibi mwa Iraq.

Alipoulizwa na shirika la habari ni muda gani utahitajika ili kufanikisha kukomboa upande wa magharibi wa mji huo, al-Abadi alisema  hawezi kusema sasa lakini akaongeza kuwa wana uwezo wa kulikomboa eneo hilo na watafanya hivyo.

Mamia ya raia walilazimika kuyahama maeneo ya jirani ya kaskazini mashariki ya Rashidiya kwa miguu wakati helkopta za Iraq zilipolizunguka eneo hilo na kuwashambulia kwa mabomu wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh.

Uchunguzi kufanyika dhidi ya ukiukaji wa haki za binadamu

Wakati huohuo Waziri Mkuu Haider al- Abadi alirudia ahadi yake ya kufanya uchunguzi dhidi ya madai ya ukiukaji wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa na vikosi vya Iraq na hatimaye kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale wote watakaobainika kuhusika.

Matamshi yake yanakuja  siku moja baada kuagiza kufanyika uchunguzi kuhusiana na vidio iliyoko katika mitandao ya kijamii inayoonyesha wanajeshi  wa vikosi vya serikali wakiwapiga na kuwaua watu watatu washukiwa wa kundi la kigaidi la Daesh mjini Mosul.

Hapo jana kamati iliyoundwa kuchunguza vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu vilivyofanyika katika mji wa Fallujah Juni mwaka jana ilikamilisha kazi yake ambapo Waziri Mkuu al- Abadi alisema kamati hiyo imewahusisha wafuasi wa kundi la wanamgambo wa kishia  na mauaji ya raia 17.

Operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul ilianza Oktoba mwaka jana kwa msaada wa mashambulizi ya anga na ushauri kutoka muungano uanaoongozwa na Marekani. Hata hivyo Waziri Mkuu al- Abadi amekanusha kuwepo vikosi vya kigeni vinavyopambana  katika mashambulizi ya nchi kavu huku akisema utawala wa Rais wa sasa wa Marekani  Donald Trump  umeahidi kuongeza msaada wake kwa Iraq.

Mwisho wa habari / 291

 

Tags