Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

25 Juni 2021

10:37:01
1153679

Ayatullah Khamenei apewa dozi ya kwanza kabisa ya chanjo ya corona ya COVIran Barekat iliyotengenezwa hapa nchini

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema leo Ijumaa amedungwa dozi ya kwanza kabisa ya chanjo ya corona ya COVIran Barekat na kusema kuwa: Kuna ulazima wa kuthamini na kuenzi fahari hii ya taifa ya kuzalisha chanjo ya Kiirani ya corona.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Baada ya kudunga chanjo hiyo ya COVIran Barekat iliyotengeneza hapa nchini,  Ayatullah Ali Khamenei amewashukuru watalamu na maafisa wote walioipa nchi hii fahari ya kitaifa kutokana na elimu, tajiriba na juhudi zao kubwa za kisayansi na kivitendo na kusema: "Awali sikupendelea kutumia chanjo isiyokuwa ya Kiirani, kwa msingi huo nilisema kwamba, nitasubiri chanjo ya Kiirani ya corona; kwa sababu tunapaswa kuthamini fahari hii ya taifa; na maadamu inawezekana kuzuia na kutibu maradhi hapa hapa ndani ya nchi, kwa nini tusiitumie?"

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, hakuna tatizo lolote kutumia chanjo ya corona iliyotengenezwa na nchi nyingine pale inapohitajika sambamba na utumiaji wa chanjo ya corona iliyotengenezwa hapa nchini, lakini tunapaswa kuheshimu na kuenzi chanjo ya Kiirani. Ayatullah Khamenei amewashukuru wanasayansi wote vijana, wachapakazi na waliofanya bidii kubwa katika uzalishaji wa chanjo hiyo ya corona na vituo vingine vinavyofanya kazi kutengeneza chanjo nyingine hapa nchini.

Ayatullah Khamenei pia amesitiza udharura wa kusajili nyaraka za kisayansi na kuchapisha makala zinazohusiana na chanjo ya corona ya COVIran Barekat na kusema: Sambamba na uzalishaji madhubuti, wa haraka na kwa wakati mwafaka wa chanjo hiyo, nyaraka zote na makala za kisayansi za chanjo hiyo pia zinapaswa kutayarishwa na kuchapishwa kwa shabaha ya kuionesha dunia kazi kubwa iliyofanyika hapa nchini. 

Chanjo ya corona ya COVIran Barekat ni matunda ya wahakiki na wanasayansi vijana wa Iran ambayo hivi karibuni iliidhinishwa kuanza kutumiwa kwa ajili ya kujikingi na ugonjwa wa COVID-19.

Kuzinduliwa chanjo hiyo kunaiweka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika orodha ya nchi sita tu duniani zinazotengeneza chanjo ya corona.  

342/