Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

18 Novemba 2022

19:11:56
1324317

Mabadiliko ya hali ya hewa kusababisha mafuriko mabaya barani Afrika

Uchunguzi uliochapishwa na gazeti moja la Marekani umebaini kuwa kuna uwezekano wa kutokea mafuriko makubwa yatakayosababisha vifo vingi barani Afrika.

Mtandao wa gazeti la Washington Post la Marekani umeripoti kuwa, watafiti wamefikia hitimisho kwamba mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na binadamu yameongeza uwezekano wa kunyesha mvua kubwa kupita kiasi  itakayosababisha mafuriko mara 80 zaidi ya yale yaliyoshuhudiwa karibuni nchini Nigeria.

Mafuriko makubwa msimu huu wa kiangazi na vuli yamewalazimisha Wanigeria milioni 1.5 kuyahama makazi yao na kuua wengine 612. Mafuriko hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 800 katika eneo la Magharibi mwa Afrika.

Watafiti kutoka Shirika la World Weather Attribution Group, ambalo linatathmini athari za mabadiliko ya tabianchi katika hali mbaya ya hewa, waligundua kuwa msimu wa mvua huko Afrika Magharibi ulikuwa na asilimia 20 zaidi ya mvua kuliko  ilivyopaswa kuwa bila mabadiliko ya hali ya hewa.

Ripoti zinaonesha kuwa, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, vipindi vifupi vya mvua kubwa, ambavyo vimezidisha mafuriko ya hivi karibuni, vimeongezeka maradufu katika eneo la Niger.

Nigeria, Niger, Cameroon, Chad na Benin ni miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi na mafuriko hayo. Takriban watu 200 walifariki dunia nchini Niger na 22 nchini Chad.

Kawaida msimu wa mvua katika eneo la Afrika Magharibi huanza mwezi Mei hadi Oktoba, lakini mwaka huu msimu huo ulianza mapema. Nigeria na Niger ndizo nchi za kwanza kukumbwa na mafuriko makubwa.

Uchambuzi huo ulihitimisha kuwa eneo hilo litakumbwa na mafuriko makubwa zaidi katika miongo ijayo.

342/