Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA-, Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ilitangaza kuwa Ukraine ilitekeleza shambulio kwa kutumia droni 91 za masafa marefu dhidi ya makaazi ya Rais Vladimir Putin katika eneo la Novgorod. Hata hivyo, mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi ilifanikiwa kuzitungua droni zote.
Mashambulizi hayo yalifanyika jioni ya Jumamosi na pia usiku uliofuata, sambamba na mazungumzo mazito yaliyokuwa yakiendelea kati ya Urusi na Marekani kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro wa Ukraine.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, droni zote zilizoshambulia ziliangushwa, na hakuna taarifa za vifo wala uharibifu uliosababishwa na mabaki ya droni hizo.
Wakati huo huo, Ikulu ya Kremlin ilithibitisha kuwa marais wa Urusi na Marekani walifanya mazungumzo ya simu jioni ya Jumatatu, ambapo ilielezwa kuwa Donald Trump alishtushwa sana na shambulio la droni la Ukraine dhidi ya makaazi ya Rais Putin.
Yuri Ushakov, msaidizi wa Rais wa Urusi, alisema kuwa Trump aliposikia habari hiyo alishtuka kwa kiwango kikubwa, akakasirika sana na kusema kuwa hawezi kufikiria hatua za “kichaa” kama hizo.
Kwa mujibu wa Ushakov, Rais Putin alimwambia Trump katika mazungumzo hayo kuwa msimamo wa Urusi katika mazungumzo ya kumaliza mgogoro wa Ukraine utapitiwa upya kufuatia hatua hiyo ambayo Moscow inaiona kama ugaidi wa kiserikali wa Kyiv.
Hata hivyo, Rais wa Urusi alisisitiza kuwa Moscow itaendelea na ushirikiano wa karibu na wa kujenga na washirika wake wa Marekani ili kutafuta njia zitakazowezesha kupatikana kwa amani.
Your Comment