Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Zubair bin Ali Wambwana, amesisitiza umuhimu wa kulinda na kuendeleza amani katika jamii, akibainisha kuwa amani ni msingi muhimu uliokithiri kusisitizwa ndani ya Qur’an Tukufu.
Akizungumza katika mafunzo yake yaliyojikita katika kuhamasisha mshikamano na utulivu wa kijamii, Sheikh Dkt. Abubakar ameeleza kuwa Qur’an imeweka bayana thamani ya amani katika nyanja zote za maisha ya mwanadamu - kuanzia mahusiano ya kifamilia, kijamii hadi ya kitaifa na kimataifa. Amesema msisitizo huu wa Qur’an unaonesha wazi kuwa amani si chaguo la hiari, bali ni nguzo ya msingi ya uhai na maendeleo ya jamii.
Katika kufafanua hoja yake, Mufti Mkuu wa Tanzania ametaja kisa cha wageni wa Nabii Ibrahim (as) kama kinavyosimuliwa ndani ya Qur’an Tukufu. Amesema kuwa wageni hao walipoingia nyumbani kwa Nabii Ibrahim (as), walimpa maamkizi ya amani, naye akajibu kwa maamkizi yale yale ya amani. Qur’an inasema:
إِذْ دَخَلُوا عَلَيْهِ فَقَالُوا سَلَامًا ۖ قَالَ سَلَامٌ قَوْمٌ مُنْكَرُونَ
“Walipoingia kwake wakasema: Amani (Salama!). Naye akasema: Amani (Salama!). Nyinyi ni watu nisiowajua.”
Sheikh Dkt. Abubakar ameeleza kuwa tukio hili linafunza kwa vitendo namna ambavyo Manabii wa Mwenyezi Mungu walivyokuwa wakitanguliza amani hata katika hali ya kutojua uhalisia wa wageni wao. Amesema kuwa majibu ya Nabii Ibrahim (as) ni ushahidi wa hali ya juu wa adabu, busara na msimamo wa Kiislamu katika kulinda amani na kuepuka migogoro.
Aidha, Mufti Mkuu amewahimiza Waislamu na jamii kwa ujumla kuitafsiri Qur’an katika vitendo, kwa kueneza lugha ya amani, kuheshimiana, na kujiepusha na maneno au matendo yanayochochea migawanyiko na chuki. Amesisitiza kuwa Salamu ya Kiislamu yenyewe kama ilivyo - As-Salaam Alaikum - ni ujumbe wa moja kwa moja wa Amani, tunaopaswa kuuishi kwa vitendo katika maisha ya kila siku.
Kwa mujibu wa Sheikh Dkt. Abubakar Zubair, jamii yoyote inayojengwa juu ya misingi ya amani, mazungumzo na kuvumiliana, huwa na uwezo mkubwa wa kufikia maendeleo ya kweli na kudumisha umoja wa kudumu. Hivyo, amewataka viongozi wa dini, wazazi, walimu na vijana kuwa mabalozi wa amani, wakitumia mafundisho ya Qur’an na Sunna kama dira ya maisha.
Mwisho, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania amehitimisha kwa kusisitiza kuwa amani ni amana kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na kuitunza ni jukumu la kila mmoja bila kujali dini, kabila au itikadi, kwa kuwa pasipo amani, hakuna mafanikio wala ustawi wa jamii.
Your Comment