Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kiongozi mkuu wa harakati ya Ansarullah ya Yemen, Sayyid Abdul-Malik al-Houthi, amesema kuwa Wahouthi wako tayari kufanya kila wawezalo kuiunga mkono Somalia, akisisitiza kuwa hawataruhusu sehemu yoyote ya ardhi ya Somalia kutumiwa na utawala wa Kizayuni kama ngome au kambi ya kijeshi.
Al-Houthi amebainisha kuwa kambi au kituo chochote cha kijeshi cha Israel kitakachoanzishwa katika eneo la Somaliland kitachukuliwa kuwa ni shabaha halali ya kijeshi, na kusisitiza kuwa Wahouthi wako tayari kuchukua hatua za moja kwa moja dhidi ya vituo hivyo.
Aidha, alionya kuwa harakati ya Ansarullah haitaruhusu Israel kujipatia nafasi ya kijeshi katika ardhi ya Somalia, akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa lengo la kulinda usalama, mamlaka na heshima ya wananchi wa Somalia.
Al-Houthi alieleza kuwa uwepo wa kijeshi wa Israel katika eneo la Pembe ya Afrika ni tishio si tu kwa Somalia bali pia kwa usalama wa kikanda, na kwamba Wahouthi wanachukulia suala hilo kuwa mstari mwekundu usiovukwa.
Ikumbukwe kuwa, moja ya sababu kuu zinazotajwa katika hatua ya Israel kuitambua Somaliland ni nafasi ya kijiografia ya eneo hilo, ambayo inaonekana kuwa na umuhimu wa kimkakati kwa Israel katika kuendesha mashambulizi dhidi ya Wahouthi wa Yemen.
Your Comment