Main Title

source : Parstoday
Jumapili

4 Juni 2023

09:30:25
1371060

BRICS: Kuarifishwa mpangilio mpya na mfumo wa kambi kadhaa za nguvu duniani

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa kundi la BRICS wamekutana katika mkutano wao wa utangulizi huko Cape Town Afrika Kusini na kutaka kuangaliwa upya mfumo wa utawala duniani pamoja na haja ya nchi huru kujitenga na nchi za Magharibi zinazotumia mabavu dhidi ya mataifa mengine.

Naledi Pandor, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, amesema lengo la kundi hilo ni kuchukua uongozi wa ulimwengu ambao, kulingana na yeye, umegawanyika na kuvurugika kutokana na mvutano wa kijiografia, kisiasa, ubaguzi na ukosefu wa usalama. Mkutano huo umeandaliwa kwa ajili ya kuratibu na kuleta uwiano miongoni mwa wanachama kwa lengo la kuandaa uwanja wa kufanyika mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za BRICS unaotarajiwa kufanyika nchini Afrika Kusini mwezi Agosti mwaka huu.

Hivi sasa, nchi tano za Russia, China, Afrika Kusini, Brazil na India ndio wanachama wa kundi la BRICS. Madhumuni ya kuundwa kundi hilo ni kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya nchi wanachama na pia kuunda taasisi za kimataifa zinazofanana na zile zilizopo hivi sasa katika upeo wa kimataifa kama vile benki za maendeleo na mfumo mpya wa biashara. Kundi hilo ambalo lilianzishwa mwaka 2009 linajumuisha zaidi ya asilimia 41 ya idadi ya watu wote duniani na zaidi ya asilimia 28 ya pato la dunia.

Wanachama wa kundi hili, ambao wengi ni nchi zinazoinukia kiuchumi, wamekuwa na mafanikio katika uwanja wa biashara katika miaka iliyopita, kwa kadiri kwamba kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia, kiwango cha hisa ya nchi wanachama wa BRICS katika ukuaji wa uchumi wa dunia mwaka huu wa 2023 kimefikia asilimia 32.1 na hivyo kupita kiwango cha nchi wanachama wa kundi la G7 ambalo linajumuisha nchi za Ujerumani, Ufaransa, Italia, Japan, Uingereza, Canada na Marekani.

Russia na China, zikiwa wanachama muhimu wa BRICS na ambazo zina jukumu muhimu katika kuimarisha uchumi wa kundi hilo, zinajaribu kubadilisha mpangilio wa sasa wa nguvu na ushawishi duniani, hasa katika uwanja wa uchumi, na hatimaye kuimarisha mfumo wa kambi kadhaa za nguvu kwa ushirikiano wa wanachama wa kundi hilo na vilevile wanachama wapya wanaotazamiwa kujiunga nalo. Katika muktadha huu, Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mambo ya Nje wa India anasema: Mkutano huu unapaswa kutuma ujumbe mzito kwamba ulimwengu wa kambi kadhaa za nguvu unaleta uwiano mpya na kwamba mbinu za zamani hazina tena uwezo wa kukabiliana na changamoto mpya.

Moja ya malengo ya kundi la BRICS ni kupambana na ubeberu wa Marekani kwenye mfumo wa uchumi wa kimataifa na kutumika sarafu nyingine mashuhuri badala ya kutumia dola katika mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi ulimwenguni. Wanachama wa BRICS wanajaribu kukomesha ubeberu wa Marekani na siasa zake za upande mmoja kwa kuongeza ushirikiano wa kiuchumi na kiwango cha uzalishaji na mauzo ya nje, pamoja na matumizi ya sarafu kama vile Yuan katika miamala ya kibiashara. Utumiaji wa dola na vikwazo kama chombo cha kutoa mashinikizo ya kiuchumi na kisiasa dhidi ya nchi ambazo hazikubaliani na siasa za ubabe za Washington katika ngazi za kimataifa ni miongoni mwa sababu ambazo zimewaleta pamoja wanachama wa BRICS.

Rais Miguel Diaz-Canel wa Cuba anasema kuhusu suala hilo kwamba: Mipango ya BRICS ya kujitenga na dola itaunda mfumo mpana zaidi wa uhusiano wa kibiashara kwa manufaa ya ulimwengu. Mahusiano ya kimataifa leo yamesimama juu ya msingi wa siasa za uchokozi na ubabe wa serikali ya Marekani ambayo daima inaziwekea nchi nyingine vizuizi, vikwazo vya kidhalimu, kuzirubuni, kuzipiga vita na kuzituhumu bila sababu yoyote ya msingi.

Utendaji mzuri na malengo ya kimaadili ya kundi la BRICS yamezipelekea nchi nyingi kama Algeria, Argentina na Iran kuomba kujiunga na kundi hilo. Pia, nchi kama Saudi Arabia, Uturuki na Misri nazo zimeonyesha hamu ya kujiunga na kundi hilo. Rais Nicolás Maduro wa Venezuela, nchi ambayo imekuwa chini ya vikwazo vikali vya Marekani kwa miaka mingi, pia amesema kuhusu suala hilo kwamba: Tunataka kuwa sehemu ya BRICS na kushiriki vilivyo katika usanifu huu mpya wa siasa za dunia. BRICS inaendelea kubadilika na kuwa sumaku kubwa ya kuwavutia wale wanaotaka ulimwengu unaozingatia amani na ushirikiano.

Mauro Vieira, Waziri wa Mambo ya Nje wa Brazil amefafanua BRICS kuwa ni utaratibu muhimu wa kuunda mpangilio mpya wa dunia yenye pande kadhaa za nguvu na kusema: Mfumo kama huo unaakisi zana na mahitaji ya nchi zinazoendelea.

Nukta nyingine muhimu hapa ni kwamba, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa BRICS wamekaribisha kurejea Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kusisitiza uwepo wa kivitendo zaidi wa jumuiya hiyo katika nyanja za kisiasa na kiuchumi. Inaonekana kwamba kwa kukubali wanachama wapya, BRICS itaibuka kuwa na nguvu zaidi na kuwa mshindani mkubwa wa Marekani na kundi la G7 katika nyanja za kimataifa.

342/