Main Title

source : Parstoday
Jumapili

4 Juni 2023

09:31:47
1371062

Kujitoa Imarati katika muungano wa baharini na Marekani; Sababu na ujumbe wake

Wizara ya Mambo ya Nje ya Imarati hivi karibuni ilitoa taarifa na kutangaza kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) miezi miwili iliyopita ulijitoa na kuacha kushiriki kwenye Muungano wa Nguvu ya Baharini kutokana na tathmini yake endelevu ya ushirikiano mzuri wa usalama na washirika wake wote.

Muungano huo wa baharini ulianzishwa mwaka 2001 Miladia ambapo awali ulikuwa na nchi wanachama 12, lakini hii leo unajumuisha vikosi vya nchi 34 na umeziweka katika ajenda yake ya kazi hatua kama kurejesha usalama, kupambana na ugaidi na pia kukabiliana na maharamia katika Bahari Nyekundu na katika maeneo ya kandokando ya Ghuba ya Uajemi. Makao makuu ya muungano huo wa baharini yako Bahrain, na yako karibu na kikosi cha tano cha manowari za Marekani na Kamandi Kuu ya nchi hiyo. 

Ni muhimu kutaja nukta kadhaa hapa kuhusu ni kwa nini Imarati imeamua kujitoa katika muungano huo. 

Nukta ya kwanza ni kuwa Imarati imejitoa katika muungano huo wa nguvu wa baharini na Marekani baada ya kuhuishwa uhusiano wa Iran na Saudi Arabia na kudhihiri umoja katika Ulimwengu wa Kiarabu kwa ajili ya kupanua mahusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa msingi huo, Imarati umefikia natija hii kwamba, isijihusishe katika hatua zilizo dhidi ya Iran. Suala hili limeashiriwa wazi katika taarifa ya karibuni ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Imarati ambayo ilieleza kuwa: "Kutokana na tathmini yetu endelevu ya ushirikiano mzuri wa usalama na wenzetu, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) miezi miwili iliyopita ulijitoa na kuacha kushirikiana na vikosi vya wanamaji vya muungano huo." 

Nukta ya pili ni hii kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) sawa kabisa na nchi nyingine za kanda hii ikiwemo Saudi Arabia umefikia natija kuwa, usalama wa eneo la Asia Magharibi hautadhaminiwa na madola ajinabi bali unaweza kudhaminiwa katika kalibu ya ushirikiano wa kieneo.  

Nukta ya tatu; hatua ya Imarati inadhihirisha pengo lililojitokeza kati ya nchi za Kiarabu na Marekani. Nchi za Kiarabu na hasa Saudi Arabia na Imarati zimetambua kuwa, kwa upande mmoja, Marekani inazitazama kwa dharau na kuzichukulia nchi hizo kama wenzo tu na katika upande mwingine, ushirikiano wa pamoja baina ya nchi hizo na Marekani pia badala ya kudhamini maslahi ya nchi hizo unaegemea katika kudhamini na kulinda maslahi ya Marekani tu. Ndio maana nchi hizo pia zikaamua kuchukua maamuzi huru zaidi katika sera zake za nje. Hivi karibuni vyombo vya habari duniani vilitoa uchambuzi kuhusu kuwa mbali Abu-Dhabi na Washington. Jarida la kiuchumi la Forbes limeandika katika ripoti yake ya uchambuzi kwamba baada ya Saudi Arabia kuna uwezekano nchi nyingine ya Kiarabu yaani Imarati ikajitoa katika kalibu ya Marekani; na kuanzia sasa Abu-Dhabi itafanya jitihada kwa ajili ya maslahi jumla ya Imarati. 

Hamid Farsi mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Misri pia ameashiria kujitoa Imarati katika Muungano wa Baharini unaoongozwa na Washington na kueleza kuwa kujitoa Imarati katika Muungano wa Baharini unaoongozwa na Marekani katika Mashariki ya Kati ni ushahidi wa wazi na wenye nguvu unaodhihirisha ukubwa na hitilafu zilizopo khususan kati ya Marekani na Imarati, na kati ya nchi hiyo ya Magahribi na nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi kwa ujumla. Imarati imetambua kuwa haitapata chochote katika muungano huo, na uamuzi iliochukua wa kujitoa kwenye muungano huo ni ishara ya malalamiko na upinzani wa nchi hiyo kwa misimamo ya Marekani. Mchambuzi huyo wa Misri aidha anaongeza kwa kusema: Matukio ya Mashariki ya Kati yanaonyesha kupungua ushawishi wa Marekani na jinsi uwepo wa nchi hiyo ulivyo na taathira hasi kwa amani na usalama wa eneo hili.

342/