Main Title

source : Parstoday
Jumapili

4 Juni 2023

09:33:34
1371064

Kuchukizwa maadui na ushindi wa kidiplomasia wa Iran katika Umoja wa Mataifa

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Alhamisi iliyopita iliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la 78 la Umoja wa Mataifa na vile vile ripota wa Kamati ya Upokonyaji na Kuzuia Usambazaji Silaha ya Baraza Kuu na pia kuwa mjumbe wa bodi ya uongozi ya kamati hiyo.

Kufuatia uamuzi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeteuliwa kuwa moja ya makamu wenyeviti watano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutoka kundi la Asia-Pacific katika kikao kijacho cha baraza hilo ambacho kitaanza shughuli zake kuanzia mwezi Septemba ujao kwa kuhudhuriwa na viongozi wa ngazi ya juu wa nchi mbalimbali duniani. Awali, nchi 56 wanachama wa kundi la Asia-Pacific zilikuwa zimeidhinisha ugombea wa Iran katika nafasi hiyo.  

Mbali na kusimamia mikutano ya Baraza Kuu lijalo la Umoja wa Mataifa, Makamu Mwenyekiti aliyechaguliwa wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, pamoja na wajumbe 5 wa kudumu wa Baraza la Usalama, wanaunda wajumbe wa Kamati Kuu, ambayo itakuwa na jukumu la kuainisha ajenda na uendeshwaji wa mikutano mbalimbali ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. 

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa aidha kwa kauli moja limemteua mgombea huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa Ripota wa Kamati ya Kupunguza na Kuzuia Uenezaji wa Silaha ya Baraza Kuu la UN na kuwa mjumbe wa bodi ya uongozi ya kamati hiyo.  

Teuzi hizo mbili zinapaswa kutajwa kama ushindi wa iana mbili kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa diplomasia. Hii ni kwa sababu katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita, Marekani na waitifaki wake walifanya jitihada kubwa katika duru za kidiplomasia ili kuzuia kuteuliwa Iran katika nyadhifa mbili hizi. Ndio maana wabunge wa Marekani na wa utawala wa Kizayuni baada ya kugonga mwamba jitihada zao hizo na kuteuliwa Iran kuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la 78 la Umoja wa Mataifa wameshindwa kuficha hasira na ghadhabu zao; ambapo wameibuka na kukariri tuhuma zisizo na msingi dhidi ya mpango wa makombora na miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani kulalamikia uteuzi huu tajwa. 

Hii ni katika hali ambayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran licha ya mashinikizo yote dhidi yake na ukwamishaji wa Marekani na waitifaki wake hivi karibuni ilipata mafanikio mengine tena kufuatia kuteuliwa Ali Bahreini Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika taasisi za kimataifa mjini Geneva Uswisi kuwa Mwenyekiti wa Kikao cha 19 cha Baraza la Kijamii la Baraza la Haki za Binadamu katika mwaka huu wa 2023. 

Ni wazi kuwa Marekani na washirika wake katika miaka ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na hasa miaka ya karibuni wamefanya kila linalowezekana ili kuhakikisha kuwa Iran inatengwa kimataifa; namiongoni mwa hatua hizo mbali na kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi Marekani na washirika wake zimefanya kila njama ili kupunguza ushawishi wa Iran katika taasisi kama Umoja wa Mataifa na nyingine za kimataifa lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa nchi yenye taathira na iliyo na ushawishi mkubwa kikanda na kimataifa imeweza kupata mafanikio ya kidiplomasia katika taasisi za kimataifa na pia katika kukuza uhusiano na nchi za Asia na majirani zake kwa kuzingatia misingi yake madhubuti na pia  serikali ya 13 kuwa na mlingano katika sera zake za nje sambamba na kupinga sera na misimamo ya magharibi katika uhusiano wa nje.   

Kwa msingi huo kuteuliwa Iran kuwa moja ya makamu wenyeviti watano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na vile vile kuwa Ripota wa Kamati ya Upokonyaji na Kuzuia Usambazaji Silaha ya Baraza Kuu la UN kunaonyesha kushindwa Marekani na washirika wake katika vita vya kidiplomasia na Iran katika taasisi za kimataifa na pia dhihirisho la mafanikio na matunda ya diplomasia ya serikali ya Jamhuri ya Kiislamu katika taasisi hizo. 

342/