Main Title

source : Parstoday
Jumapili

4 Juni 2023

09:36:26
1371068

Sheikh Zakzaky: Bado tunahitaji fikra za Imam Ruhullah Khomeini

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) ametangaza kuwa, licha ya kupita miaka 34 tangu kuaga dunia Imam Ruhullah Khomeini, fikra za mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bado ziko hai.

Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye alikuwa akizungumzia ushawishi wa fikra za mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kifo cha Imam Khomeini (RA), amesema katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari wa Iranpress mjini Abuja kwamba bado tunahitajia mawazo na fikra za Imam Khomeini.

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesisitiza kuwa fikra za Imam Khomeini ziko hai siku zote, kwa sababu Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anafuata nyayo zake.

Kuhusu maendeleo ya kisayansi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran chini ya kivuli cha vikwazo, Sheikh Zakzaky amesema Iran haitegemei nchi za nje na hii ndiyo sababu ya maendeleo yake.

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema Iran inasonga mbele kwa kutegemea maarifa ya wataalamu na wasomi wa ndani na kutokana na kukata utegemezi kwa nchi za kigeni, na vijana wa Iran ni wavumbuzi katika nyanja mbalimbali za kisayansi.

Sheikh Ibrahim Zakzaky amesisitiza kuwa, kwa mujibu wa maendeleo ya kisayansi ya Iran, Jamhuri ya Kiislamu inaweza kulinganishwa na nchi zilizoendelea.

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pia amezungumzia suala la kuhuishwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Iran na Saudi Arabia na kusema: Tukio hili ni maendeleo mazuri, kwa sababu Wasaudia wametambua kwamba uhusiano wao na Magharibi daima umekuwa ni kwa maslahi ya madola ya Magharibi. 

Amesisitiza kuwa, nchi za Magharibi zinataka rasilimali na utajiri wa Saudi Arabia tu, na hapana shaka kuwa kurejeshwa uhusiano kati ya Riyadh na Tehran kutaifanya Saudi Arabia isitegemee tena nchi za Magharibi na ijitegemee yenyewe.

342/