Main Title

source : Parstoday
Jumapili

4 Juni 2023

09:39:12
1371071

Ayatullah Issa Qassim: Wananchi wa Bahrain hawatasalimu amri

Ayatullah Issa Qassim, kiongozi wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia nchini Bahrain ametangaza kuwa, wananchi wa Bahrain katu hatawasalimu amri mbele ya dhulma na ukandamizaji dhidi yao.

Kiongozi huyo wa Waislamu wa Kishia nchini Bahraina amesema hayo katika radiamali yake kufuatia kunyongwa vijana wawili wa Kibahrain huko Saudi Arabia na kueleza kwamba, ishara ya kutosalimu amri wananchi wa Bahrain zinaonekana wazi kutokana na kusimama kwao kidete kila uchao mkabala wa dhulma na ukandamizaji wa utawala wa Bahrain.

Upinzani na maandamano yameendelea kushuhudiwa nchini Bahrain kulalamikia hatua ya Saudia ya kuwanyongwa vijana  wawili wa Kibahrain Sadiq Thamir na Ja'afar Sultan.

Maandamano yameshuhudiwa katika eneo walipozaliwa vijana hao ambapo waandamaji wametoa wito wa kukabidhiwa miili ya mashahidi hao.

Harakati ya Kiislamu ya al-Wifaq imesema kuwa, Saudia imefanya kosa kuwanyonga vijana hao na kwamba, kitendo hicho kimetekelezwa kwa matashi ya kisiasa bila kujali vigezo vidogo kabisa vya kisheria.

Tangu Februari 14 mwaka 2011 Bahrain imekumbwa na vuguvugu la harakati za mapinduzi ya wananchi dhidi ya utawala wa ukoo wa Al Khalifa. Wananchi wa Bahrain wanataka kuwa huru, kutekelezwa uadilifu, kukomeshwa ubaguzi na kuingia madarakani serikali itakayochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. 

Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International lililitangaza hivi majuzi kwamba, utawala wa kifalme wa Bahrain umeendelea kukandamiza uhuru wa kujieleza na kuendelea kuwashikilia wafungwa raia wanaoukosoa utawala huo.

342/