Main Title

source : Parstoday
Jumanne

6 Juni 2023

20:19:10
1371523

Kuongezeka idadi ya wahitaji wa misaada ya kibinadamu nchini Afghanistan

Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imetangaza katika taarifa yake kwamba, tathmini mpya inaonyesha kuwa, idadi ya watu wanaohitajia misaada ya kibinadamu nchini Afghanistan imeongezeka.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu 500,000 wameongezeka katika idadi ya wahitaji wa misaada ya kibinadamu kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu hadi mwezi huu wa mwezi Juni. Kabla ya hapo pia, Umoja wa Mataifa ulitangaza kwamba, idadi ya watu wanaohitajia misaada ya kibinadamu nchini Afghanistan imeongezeka na kufikia milioni 28.3. Hivi sasa kwa tangazo hili la OCHA idadi ya raia wanaohitajia misaada ya kibinadamu nchini Afghanistan imefikiia milioni 29. Hii ina maana kwamba, katika kipindi cha utawala wake wa miaka miwili tangu lishike tena madarakan nchini Afghanistan, kundi la wanamgambo wa Taliban halijaweza kutatua matatizo ya wananchi wa nchi hiyo hususan matatizo ya kimaisha na mahitaji ya chakula. Wajuzi wa mambo wanasema kuwa, Taliban imeshindwa kuchukua hatua za maana kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wananchi wa Afghanistan hasa tatizo la uhaba wa chakula.

Hata kama wavamizi wa Kimarekani na washirika wake katika kipindi cha miongo miwili cha uwepo wao nchini Afghanistan walibomoa na kuharibu kabisa miiundomsingi ya kiilimo na uchumi, lakini wanamgambo wa Taliban walikuwa na fursa katika kipindi cha miaka hii miwili tangu waingie madarakani ya kuboresha ushirikiano na mataifa jirani na hivyo kuandaa uwanja na mazingira ya kuimarisha nafasi ya nchi hiyo kimataifa kwa minajiili ya kuyapatia ufumbuzi matatizio ya wananchi hususan uhaba wa bidhaa za chakula.

Asadullah Zairi, mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: Afghanistan ina uwezo na mazingira mwafaka kabisa ya kupatia ufumbuzi mahitaji ya wananchi ambapo kwa kuandaa mipango mizuri ya kilimo inaweza kufikia lengo hilo. Afghanistan ina ardhi yenye rutuba na maji ya kutosha ambapo kutumia nyenzo hizo mbili sambamba na kuwa na irada thabiti inawezekana kuyapatia ufumbuzi matatizo ya wananchi katika uga wa uhaba wa chakula.

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, kuanzia mwisho mwa mwaka jana (2022) hadi sasa umefanikiwa kusaidia kwa akali watu milioni 17.3 wa Afghanistan kupitia dola milioni 924 za misaada ya kimataifa. Inaonekana kuwa, jamii ya kimataifa nayo, haitoa misaada ya kifedha kama inavyotakiwa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya dharura ya wananchi wa Afghanistan. Moja ya sababu za hilo, ni kukosa shauku na kukata tamaa kutokana na matukio ya nchini Afghanistan.

Ismail Bagheri, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na hili kwamba:  Ili Afghanistan iweze kupata misaada ya kimataifa inahitajia kuliko wakati wowote ule kujenga imani ya kieneo na jamii ya kimataifa kwake, lakini inavyoonekana serikali ya Taliban haijafanikiwa katika hili.

Hii ina maana kwamba, Wanamgambo wa Taliban wakiwa ndio watawala nchini Afghanistan kwa kukubali kubeba dhima mkabala na wananchi, inapaswa kutazama upya mipango yake ya kisiasa ambapo sambamba na kuwafanya watu ndani ya nchi wawe na imanii nao ifanye juhudi za kutekeleza na kuimarisha siasa za ujirani mwema.

Alaa kulli haal,  kuendelea matatizo ya kimaisha na uhaba wa chakula siyo tu kwamba, hayo yanatakuwa tishio kwa maisha ya wananchi wa Afghanistan, bali yatapelekea pia kuongezeka wimbi la wahajiri.

Tangazo la kuendelea na kuongezwa misaada ya kibinadamu kwa wananchii wa Afghanistan licha ya kuwa hilo linabainisha kutoa umuhimu jamii ya kimataifa kwa hali ya nchi hiyo, lakini hilo haliwezi kuwa dawa mujarabu kwa mahitaji na matarajio ya wananchi ambao wanaweza kudhamini mahitaji yao kwa urahisi kabisa kupitia hima na juhudi katika fremu ya kuweko mzunguko wa kiuchumi nchini kwao.