Main Title

source : Parstoday
Jumanne

6 Juni 2023

20:19:37
1371524

UN 'yaguswa' na ukatili wa Israel wa kumuua mtoto wa miaka 2

Umoja wa Mataifa umelaani mauaji ya mtoto mdogo wa Kipalestina yaliyofanywa na vyombo vya usalama vya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tor Wennesland, Mratibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa kwenye Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati amesema, "Nalaani na nimesikitishwa na kifo cha ghafla cha mtoto wa miaka miwili wa Kipalestina, aliyejeruhiwa katika ufyatuaji risasi wa vikosi vya usalama vya Israel huko Al-Nabi Saleh."

Ameeleza kuwa, raia na hususan watoto wadogo wameendelea kuwa wahanga wa mgogoro huo, huku akitoa mwito kwa mamlaka husika za utawala haramu wa Israel kuwawajibisha waliotenda jinai hiyo.

Wizara ya Afya ya Palestina imethibitisha kifo cha mtoto huyo aliyekuwa na miaka miwili kwa jina Mohammad Tamimi, aliyejeruhiwa vibaya na risasi za Wazayuni siku ya Alkhamisi mjini Al-Nabi Saleh karibu na mji Ramallah, eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Wakati huo huo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetoa wito wa kutambuliwa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watoto wa Kipalestina kuwa ni uhalifu, na kuwafungulia mashitaka wanaofanya jinai hizo.

Harakati hiyo imesisitiza kuwa, vitendo vya kigaidi vya utawala unaoikalia kwa mabavu Quds dhidi ya watoto wa Kipalestina vinaendelea kupitia mzingiro wa kikatili wa Ukanda wa Gaza, kwa kadiri kwamba tangu mwanzoni mwa mwaka huu, zaidi ya watoto na barobaro 28 wasio na hatia wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa utawala huo.

342/