Main Title

source : Parstoday
Jumanne

6 Juni 2023

20:20:49
1371526

Balozi za Iran na Saudia zinafunguliwa rasmi leo na kesho, Tehran na Riyadh

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, balozi za Saudi Arabia na Iran zinafunguliwa rasmi leo Jumanne na kesho Jumatano katika miji mikuu ya nchi hizi mbili ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya pande mbili ya kurejesha kikamilifu uhusiano wao wa kidiplomasia.

Nasser Kan'ani Chafi amesema hayo na kuongeza kuwa, ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Riyadh na ubalozi wake mdogo mjini Jeddah, Saudi Arabia zilianza kufanya kazi kabla ya mahujaji wa Iran kuanza kuelekea kwenye ardhi za Wahyi huko Saudia kwa ajili ya ibada tukufu ya Hija. Zilianza kazi mapema ili kuwarahisishia huduma mahujaji wa Kiirani. Kinachofanya hivi sasa ni kufunguliwa rasmi balozi hizo kwa kuhudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu wa Wizara za Mambo ya Nje za nchi hizi mbili.

Tarehe 10 Machi 2023, nchi mbili kubwa katika Ulimwengu wa Kiislamu za Iran na Saudi Arabia zilifikia makubaliano ya kurejesha uhusiano baina yao kwa upatanishi wa China ukiwemo uhusiano wa kidiplomasia. Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya miaka 7 ya Saudia kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran. 

Taarifa hiyo iliyomnukuu Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Iran imesema pia kwamba, juzi Jumapili, Hossein Amir Abdolahia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alizungumza kwa simu na msimamiaji wa muda wa ubalozi wa Iran mjini Riyadh kuhusu hali halisi ilivyo hivi sasa na maandalizi ya kufunguliwa rasmi ubalozi wa Iran mjini humo na ule ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu wa mjini Jeddah, Saudi Arabia.

342/